Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.
28 Januari 2010Mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan unafanyika mjini London leo , pamoja na masuala mengine, kujadili njia za kuwakaribia wataliban.
Wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanatoa
maoni yao juu ya mkutano huo.
Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya hotuba
iliyotolewa jana na rais Shimon Peres wa Israel
kwenye bunge la Ujerumani katika maadhimisho
ya mwaka wa 65 tokea kukombolewa kwa watu
waliokuwa wamefungwa katika kambi ya
Auschwitz nchini Poland.
Juu ya mkutano unaojadili suala la Afghanistan
mjini London gazeti la Rhein-Necker linasema ,
kuwa mkutano huo hautaisogeza Afghanistan
kwenye hatua ya amani, badala yake mkutano
huo unatumiwa na nchi za magharibi kwa
maslahi yao ya kisiasa.Gazeti hilo linaeleza kuwa
mkutano huo ni jukwaa la kisiasa linalotumiwa
na nchi za magharibi kwa lengo la kufafanua
mkakati wa kujiondoa Afghanistan.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung linatilia maanani
kwamba rais Karzai anajaribu kutafuta njia ya
kuwakaribia wataliban. Gazeti linasisitiza
kwamba hilo ni jukumu la rais huyo kwa sababu
haiwezekani kwake kuendelea kwa muda mrefu
zaidi kutegemea kulindwa na majeshi ya nchi za
nje. Gazeti hilo linaeleza kwamba
kinachowezekana kufanyika nchini Afghanistan
ni kujaribu kuwaingiza wataliban katika jamii na
kujaribu kuwatengenaisha na alkaida; lakini
zaidi ya hayo hakuna kinachoweza kufanyika
nchini humo.
Gazeti la Märkische Oderzeitung linazungumzia juu ya mkutano uliofanyika jana , pia mjini London, kuhusu Yemen. Gazeti hilo linasema Yemen imegeuka kuwa nchi isiyokuwa na matumaini kama Somalia kwa sababu kwa muda mrefu, hakuna alietaka kujua kilichokuwa kinaendelea katika nchi hiyo. Lakini sasa wakati dunia inataka kujua kinachotokea, mambo yameshaenda mrama.
Umasikini unaongezeka kutokana na kupungua
kwa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta.
Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung
anasema umasikini ndio unaowafanya watu
zaidi na zaidi wajiunge na makundi ya
wanaitikadi kali wa kiislamu. Gazeti linasema,
ndiyo serikali ipo nchini humo, lakini inazidi
kupoteza udhibiti wa nchi.
Rais Shimon Peres wa Israel jana alilihutubia
bunge la Ujerumani katika maadhimisho ya
mwaka wa 65 tokea kukombolewa kwa kambi ya
Auschwitz iliyotumika kuwaangamiza maalfu kwa
maalfu ya watu na hasa wayahudi. Katika hotuba
yake rais huyo alitoa mwito wa kuendelea
kuwakumbuka wahanga wa Auschwitz. Gazeti la
Kieler Nachrichten linaeleza kuwa sababu ya
kutoa mwito huo ni kwamba wapo watu nchini
Ujerumani wanaofikiri kwamba kumbukumbu juu
ya maangamizi ya wayahudi siyo jambo la
lazima sana. Lakini mhariri wa gazeti la
Aachener anasema asietaka kuyakumbuka
maangamizi ya wayahudi hasikii vizuri.
Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza umuhimu wa hotuba ya rais Peres pia kutokana na kutambua ukweli kwamba wapo watu nchini Ujerumani wanaojaribu kufananisha unyama waliofanyiwa wayahudi na masaibu ya wapalestina.
Mwandishi/Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.
Mhariri/Othman Miraji