Mjadala juu ya Afghanistan.
12 Januari 2010Mwenyekiti wa baraza la kanisa la kiprotestanti nchini Ujrumani, Askofu Margot Käßmann, amesema hatabadili msimamo wake wa kuikosoa sera ya serikali ya Ujerumani kuhusu Afghanistan. Askofu Käßmann amesisitiza hayo pia baada ya kukutana na waziri wa ulinzi.
Magazeti ya Ujerumani leo yanazungumzia msimamo wa askofu huyo katika safu zao za maoni.
Gazeti la Mitteldeutsche Zeitung linasema wakristo hawajiulizi kwa mara ya kwanza juu ya mchango gani ambao wao na nchi yao wanaweza kutoa nchini Afghanistan ili kuifanya hali iwe bora daima, sambamba na kuwaondolea rutuba magaidi wa kimataifa.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa hakuna anaekana nia njema au ujasiri wa wanajeshi.Lakini kila mtu, awe mkristo ama la ,anayo haki,ya kuuliza iwapo kupigana vita ndiyo njia ya kudumisha amani.?
Juu ya msimamo wa Askofu Käßmann wa kuikosoa sera ya serikali gazeti la Rhein-Necker linasema ni kwa njia ya kuruhusu mjadala wa hadhara juu ya manufaa ya vita vya nchini Afghanistan na juu ya matayarisho ya kuyarudisha nyumbani majeshi, kwamba itawezekana kwa wananchi wa Ujerumani kuiunga mkono serikali yao . Gazeti linasema waziri wa ulinzi wa Ujerumani anatambua hayo na ametafuta mwafaka na Askofu Käßmann, kwani Askofu huyo anajua anachosema.
Gazeti la Münchner Merkur linatilia maanani hatua ya busara iliyochukuliwa na waziri wa ulinzi, Karl-Theodor zu Guttenberg kumwalika askofu huyo kwa ajili ya mazungumzo. Gazeti hilo linaeleza kuwa waziri huyo amefanikiwa kupunguza makali ya mihemko juu ya vita vya Afghanistan bila ya kumwathiri mwakilishi huyo wa kanisa ambaye ni maaruf. Mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anasema kufanyika kwa mazungumzo ni ushindi kwa kila upande- askofu huyo ameweza kujua matatizo yaliyopo katika mikakati ya kijeshi na waziri zu Guttenberg ameweza kutathmini msimamo wa kanisa juu kutetea maadili.
Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anasema hakuna atakaeharibikiwa , ikiwa askofu Käßmann atawasiliana na jeshi nyumbani, na kwenye uwanja wa mapambano nchini Afghanistan.
Mhariri anafafanua kwa kueleza kwamba Kanisa kama jumuiya ya kutetea amani, lina haki ya kuuliza maswali yanayowakera wananchi hapa nchini. Kwa mfano, wanajeshi wa Ujerumani wanafanya nini nchini Afghanistan, kwa nini wapo huko na kwa muda gani ? Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anatilia maanani kwamba waziri wa ulinzi zu Guttenberg amemwalika Askofu Käßmann aongozane naye katika ziara ya kuyatembelea majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan.
Hata hivyo,mhariri anasema mashaka aliyokuwa nayo Askofu huyo juu ya vita vya Afghanistan hayataondoka kwa kufanya ziara hiyo.
Na gazeti la Braunschweiger linakumbusha kwamba wanajeshi na raia kadhalika ,wanakufa nchini Afghanistan na pana tishio la Taliban. Kwa hiyo mhariri wa gazeti hilo anasema masuala hayo yote yanapaswa kujadiliwa, badala ya kutumbukia mnamo vita vya imani, ati kwa kuwa Askofu amezungumzia suala la Afghanistan.
Mwandishi /Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri/Miraji Othman