1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya wanaharakati wa mazingira

Abdu Said Mtullya7 Novemba 2013

Pamoja na masuala mengine wahariri wanauzungumzia mkutano wa kilele juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na sakata linalowakabili watetezi wa mazingira nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/1ADUo
Mwanaharakati wa kutetea mazingira katika mahabusi
Mwanaharakati wa kutetea mazingira katika mahabusiPicha: picture-alliance/AP/Greenpeace International

Gazeti la "Rheinpfalz" linatoa maoni ya mkutano wa dunia juu ya mabadiliko ya tabia nchi unaofanyika nchini Poland. Mhariri wa gazeti hilo anasema wajumbe kwenye mkutano huo watapaswa kufanya bidii ili mkataba wa dunia juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ufikiwe mwaka wa 2015.

Mhariri huyo anasema nchi kama Marekani na China ambazo hadi sasa zimekuwa zinasimama kando lazima nazo zijumuike.Lakini msingi wa mafanikio ni msimamo thabiti wa Umoja wa Ulaya. Bara la Ulaya litapaswa kuongoza juhudi za kufikia kwenye lengo hilo.

Wanaharakati wa ulinzi wa mazingira

Gazeti la "Sächsiche"linatoa maoni juu ya kesi inayowakabili wanaharakati wa kutetea mazingira waliowekwa mahabusi katika jela za Urusi.

Mahakama ya kimataifa ya mjini Hamburg,ya sheria za baharini, inapaswa kutoa uamuzi juu ya kesi hiyo. Lakini Urusi haikupeleka mwakilishi. Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema, Mahakama ya kimataifa ya mjini Hamburg ilitoa fursa kwa pande zinazohusika kuhudhuria kesi ambapo mahakama iinapaswa kutoa uamuzi juu ya kuachiwa kwa meli na kwa wanaharakati 30 waliowekwa mahabusi nchini Urusi. Lakini kwa bahati mbaya Urusi haikuonyesha nia ya kufika mahakamani.

Mhariri wa gazeti hilo anahoji kwamba mashtaka ya Urusi dhidi ya wanaharakati hao yametiwa chumvi mno. Watu hao walitaka tu kupatikana kwa habari za uwazi juu ya shughuli za uchimbaji wa mafuta zinazofanywa na kampuni za Urusi.Jee kwa sababu hiyo tu, wapewe vifungo jela.?

Mhariri wa gazeti la "Osnarbrücker" pia anatoa maoni juu ya kesi inayowakabili wanaharakati wa kutetea mazingira iliyoanza hapo jana kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini Hamburg.Anasema katika siku ya kwanza tu mambo yameenda mrama. Sababu ni kwamba katika upande mmoja wahusika muhimu, yaani Warusi, hawakufika mahakamani. Na katika upande mwingine ni wanaharakati wenyewe. Swali ni iwapo hatua waliyoichukua haikuvuka mipaka.Hata hivyo litakuwa jambo zuri ikiwa Urusi itawakilishwa mahakamani.

Meya mpya wa New York

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia juu ya kuchaguliwa Meya mpya wa New York.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba jiji la New York litakuwa na meya kutoka chama cha Demokratik,baada ya kupita miaka 20. Mhariri wa gazeti hilo anasema mengi mazuri yalifanyika wakati wa uongozi wa Meya alietangulia Michael Bloomerg. Hata hivyo umefika wakati wa kuleta mabadiliko katika jiji la New York.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Saumu Yusufu