Umasikini waongezeka barani Ulaya
29 Oktoba 2015Gazeti la "Stuttgarter" linasema umasikini ni mkubwa katika nchi zinazoitwa za migogoro ,Ugiriki, Uhispania na Ureno. Mhariri wa gazeti hilo anasema pana hatari ya rika zima kuachwa nyuma katika nchi hizo. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba vijana hao hawana elimu, ajira wala matumaini.
Gazeti la "Stuttgarter" linasema ikiwa bara la Ulaya linataka udumisha amani ya kijamii litapaswa kuchukua hatua thabiti ili kuirekebisha hali hiyo. Na jambo muhimu sana ni kuekeza katika elimu na utafiti.
Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza kwamba kwa muda wa miaka mingi wanasiasa wamekuwa wanalalamika kwamba vijana wa bara hilo hawayazingatii maadili ya kiulaya.Kwa hivyo,anasema juhudi za kupambana na maonevu ya kijamii itakuwa fursa ya kuiimarisha Umoja wa Ulaya.
Naye mhariri wa Allgemeine anasema takriban thuluthi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 wamekumbwa na umasikini. Mhariri huyo anahofia kwamba vijana hao wanaweza kuwekwa kando na kuachwa nyuma daima. Lakini anakumbusha kuwa vijana hao ndio mustakabal wa bara la Ulaya. Ikiwa wataachwa nyuma kiuchumi, utulivu wa kijamii utakuwamo mashakani.
Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter " anasema ingawa Ujerumani ina idadi ndogo ya watu wasiokuwa na ajira,viongozi hawapaswi kuridhika kwa sababu kazi nyingi wanazofanya vijana nchini Ujerumani ni zile za mikataba mifupi na za mishahara ya chini. Mhariri wa "Stuttgarter" anasema hiyo ni changamoto kubwa.
Lazima kuing'oa mizizi ya ukimbizi
Gazeti la "Freie Presse" linasema katika mjadala juu ya mgogoro wa wakimbizi, mara nyingi viongozi wanasisitiza juu ya kutafakari mizizi inayosababisha tatizo la ukimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema mtazamo huo ni wa busara lakini siyo rahisi kuchukua hatua. Gazeti la "Freien Presse" linasema maneno matamu hayatoshi.
Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa wa kuizingatia mizizi ya ukimbizi.Gazeti la "Freie Presse" linaeleza kuwa maneno hayo ni ya kustarehesha baraza.Mhariri wa gazeti hilo anasema kinachotakiwa ni hatua thabiti za kulikabili tatizo la ukimbizi.
Deutsche Zeitungen.
Mwandishi:Mtullya Abdu.
Mhariri:Yusuf Saumu