Maoni ya wahariri juu ya ukosefu wa ajira
3 Aprili 2013Gazeti la "Donaukurier" linasisitiza kwamba hali ni ya maafa, na hasa miongoni mwa vijana. Na jambo baya zaidi,anasema mhariri wa gazeti hilo, ni kwamba hakuna dalili za matumaini katika siku za karibuni.
Mhariri wa gazeti la"Freie Presse" anazishauri serikali za Ulaya juu ya kuchukua hatua ili kulikabili tatizo la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana.Mhariri huyo anasema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, na hasa katika nchi zinazokabiliwa na mgogoro wa madeni unazidi kuwa tatizo.
Hiyo ndiyo sababu kwamba viongozi barani, Ulaya wanapaswa kuchukua hatua za haraka kulikabili tatizo hilo. Njia ya ufanisi ya kulikabili tatizo hilo ni kuzitekeleza sera zitakazoleta ustawi wa uchumi ,sambamba na kufanya maguezi katika mfumo wa mafunzo ya kazi kwa vijana. Mhariri huyo amesema yapasa kutilia maanani kwamba mustakabal wa bara la Ulaya unawategemea vijana.
Sera za kunaba matumizi:
Mhariri wa gazeti la "Südwest Presse" anaonya dhidi ya kushikilia sera za kubana matumizi.Anaeleza kuwa kwa kadri sera za kubana matumizi zinavyoendelea kung'ang'aniwa katika nchi za kusini mwa Ulaya vivyo ndivyo ukosefu wa ajira utakavyoendelea, na hasa miongoni mwa vijana.Jambo la kukasirisha ni kwamba viongozi wa nchi za Ulaya wanazungumza sana juu ya mipango ya kuleta ajira,lakini ukweli ni kwamba hawafanyi lolote. Swali ni kwamba ,vipi nchi zenye madeni ,za kusini mwa Ulaya, zitaweza kuitekeleza mipango ya kuleta ajira, ikiwa nchi hizo zinazidi kuzama katika madeni?
Tahadhari kwa Ujerumani:
Gazeti la "Neue Osnabrücker" linaitahadharisha Ujerumani juu ya mgogoro wa madeni unaozikabili nchi kadhaa katika Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anasema, kwa sasa Ujerumani bado ni imara, lakini haina maana kwamba haitaweza kuguswa na mgogoro siku moja. Mhariri anafanua kwamba mgogoro wa mabenki na madeni umesababisha athari kubwa,kama ilivyoshuhudiwa kwenye soko la ajira .Takwimu zinathibitisha kuwa nchi za Ulaya zinazidi kufarakana.
Soko la ajira nchini Ujerumani bado ni imara,kutokana na mageuzi yaliyofanywa mnamo miaka ya nyuma. Hali ni tofauti katika nchi za kusini mwa Ulaya.Nchi hizo zimenasa katika dimbwi la matatizo ,na hazijui namna ya kujinasua. Kwa mtazamo wa Ujerumani, mgogoro wa madeni bado ni tatizo la wengine.Lakini hayo hayana maana kwamba Wajerumani hawayajali matatizo ya wengine. Wanajua kwamba udhaifu wa kiuchumi katika nchi nyingine ni jambo la wasi wasi kwa uchumi wa Ujerumani..
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo