1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton apaswa kuwa macho

28 Julai 2016

Katika tahariri zao wahariri wa magazeti wanatoa maoni ya ukimya wa Kansela Merkel baada ya kutokea mashambulio yakigaidi.Pia wanamtahadharisha linton juu ya Donald Trump.

https://p.dw.com/p/1JX96
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/C.Koall

Katika siku za hivi karibuni Ujerumani ilishuhudia mashambulio kadhaa ya kigaidi. Hata hivyo kiongozi wa nchi, ,Kansela Merkel aliamua kunyamaza kimya.

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasema alichofanya Kansela Merkel siyo jambo la kawaida. Mhariri huyo anaeleza kwamba hakuna jambo baya kwa mwanasiasa kama kupoteza hisia juu ya masuala yanayowagusa wananchi . Anasema siasa ya tahadhari ambayo Bibi Merkel amekuwa anaifuata kwa muda mrefu ndiyo msingi wa mafanikio yake.

Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasema siasa hiyo imegeuka kuwa ya uoga na ya kujihami.

Naye mhariri wa "Badische Neueste Nachrichten" anatilia maanani kwamba upepo ulikuwa unavumia katika upande wa Kansela Merkel wakati idadi ya wakimbizi, waliokuwa wanaingia nchini Ujerumani, ilipoanza kupungua.Lakini mhariri huyo anasema matukio ya hivi karibuni yamebadilisha kila kitu.

Hakuna uhakika iwapo mkataba uliofikiwa na Uturuki utaendelea kutekelezwa.Kwa mujibu wa mkataba huo Uturuki itawapokea wakimbizi wanaorudishwa, na kwa upande wake itapatiwa fedha kutoka Umoja wa Ulaya.

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" pia linatilia maanani kwamba siasa ya tahadhari iliyomletea Kansela Merkel mafanikio sasa inaonekana kutokuwa tena ya busara na badala yake imegeuka kuwa siasa ya kujificha.

Hillary Clinton anapaswa kuwa macho

Gazeti la "Mittelbayerische " linamzungumzia Hillary Clinton,mwanamke wa kwanza katika historia ya Marekani kuteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha urais. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anamtahadharisha Clinton kwa kusema kwamba mshindani wake ni hodari sana kwa kutupisha masumbiwi ya chini ya mkanda.

Mgombea urais wa chama cha Demokratik Hillary Clinton
Mgombea urais wa chama cha Demokratik Hillary ClintonPicha: picture-lliance/dpa

Mhariri huyo anamshauri mgombea huyo wa chama cha Demokratik kutuama katika tajiriba zake za uwezo wa kazi katika kampeni yake. Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche" pia anamwambia Hillary Clinton awe mwangalifu juu ya mshindanani wake wa chama cha Republican, Donald Trump.

Kwa muda mrefu Donald Trump hakuwa anatiliwa maanani na watu wengi kama jinsi vile ilivyokuwa kwa Angela Merkel. Mhariri huyo anakumbusha kwamba laiti ungelikuwa ni utabiri wa wataalamu wa masuala ya kisiasa tu, basi Trump asilingefika alipofika sasa. Na ndiyo sababu asilani Clinton asifanye ajizi.

Clinton asijidanganye kwamba inatosha kuzungumzia tu juu ya sera za busara.Mhariri wa "Mitteldeutsche" anasisitiza kwamba Marekani ni nchi iliyogawanyika.

Baba Mtakatifu akutana na vijana wa dunia

Vijana wa kikatoliki kutoka duniani kote wanakutana mjini Krakow ,Poland kuadhimisha "Siku ya vijana Duniani".

Mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten" anasema Baba Mtakatifu Francis anaeshiriki kwenye kongamano la vijana hao atajaribu kuwapa moyo kwa njia ya sala ili washiriki katika juhudi za kuijenga dunia ya amani na haki. Amani inastawi kwa hatua fupi fupi, na inakuja kidogo kidogo.Bila ya amani ya kidini hapatakuwapo na amani duniani.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo