Sakata la ujasusi
25 Juni 2015Juu ya mvutano baina ya Ugiriki na wakopeshaji wake wa kimataifa mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anasema kwa vyovyote vile itakavyokuwa,Ugiriki itahitaji msaada kutoka Umoja wa Ulaya bila ya kujali iwapo nchi hiyo itaendelea kuwamo katika ukanda wa sarafu ya Euro ama la. Lakini ikiwa Ugiriki itajiondoa kwenye Euro, walanguzi wa fedha ndiyo watakaokuwa na usemi.Watapiga chuku juu ya uwezekano wa nchi nyingine kujitoa kwenye umoja wa sarafu ya Euro.Na hilo litakuwa pigo kwa Ulaya.
Sakata la ujasusi
Tokea kubainika kwamba Marekani imewapeleleza marais wa Ufaransa,Ufaransa sasa inataka kuwepo nidhamu katika shughuli za ujasusi baina ya nchi washirika. Juu ya sakata hilo gazeti la "Badische " linasema pana haja ya kuwapo ukweli juu ya suala hilo.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa, Ufaransa imeonyesha msimamo mkali ili kuwaonyesha watu wake kwamba serikali yao siyo dhaifu.Lakini mhariri wa gazeti la "Badische" anasema ukweli ni kwamba halitakuwa jambo la manufaa kwa Ufaransa kujaribu kuzikwamisha kazi za mashirika ya ujasusi ya Marekani.
Sawa na Ujerumani, Ufaransa inahitaji kushirikiana na Marekani katika shughuli za ujasusi. Hata hivyo mhariri anatilia maanani kwamba lingekuwa shauri bora iwapo Marekani ingelikuwa na subira kwa washirika wake wa barani Ulaya.
Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anasema kashfa hiyo ya ujasusi baina ya Ufaransa na Marekani pia inaweza kuwa na manufaa. Kashfa hiyo inathibitisha umuhimu mkubwa wa kuzilinda siri kwa uthabiti, na pia umuhimu wa kuwadhibiti wale wanaozilinda siri hizo.
Ufaransa imo mbioni kufanya mabadiliko katika mfumo wa ujasusi kwa sababu imesema mabadiliko hayo yataiwezesha nchi hiyo kupambana na magaidi kwa ufanisi zaidi. Lakini mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anasema, hata kama mashirika ya ujasusi nchini humo yangelipewa mamlaka zaidi, yasingeliweza kuyazuia mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa nchini humo mwanzoni mwa mwaka huu.
Gazeti la "Neue Osnabrücker" linatoa maoni juu ya sera ya Hungary kuhusu wakimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema Umoja wa Ulaya sasa unapitia kipindi kigumu. Anasema Umoja huo wa nchi 28 unatishiwa.
Haungary haitaki wakimbizi
Viongozi wa serikali waliozama katika sera za kitaifa wanazidi kujitokeza. Hali hiyo imejitokeza dhahiri kuhusiana na suala la kugawana jukumu la kuwahudumia wakimbizi.Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker " anasema anatumai kwamba Hungary itaibadilisha sera yake juu ya wakimbizi ya kutaka kujenga ukuta ili kuwazuia wakimbizi hao kuingia nchini. Katika tahariri yake gazeti hilo pia limeitaka Halmashauri ya Umoja wa Ulaya iipinge sera hiyo.
Gazeti la "Westfälische Nachrichten linaizungumzia ziara ya Malikia Elizabeth wa 2 wa Uingereza nchini Ujerumani.Mhariri huyo anasema wakati Malkia anawapungia mkono wakaazi wa jiji la Berlin na wakati wakaazi hao wanajibu kwa kupepea bendera kwa Malikia, shughuli muhimu za kisiasa zinafanyika katika vyumba vya faragha.
Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linatilia maanani kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanafanya vikao kuuzumgumzia mustakabali wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anasema Umoja wa Ulaya unaihitaji Uingereza na Uingereza inauhitaji Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Iddi Ssessanga