1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya tathmini ya Moody's

Abdu Said Mtullya26 Julai 2012

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya Shirika la kupima uwezo wa nchi wa kifedha na kiuchumi Moody's. Shirika hilo limeyateremsha matarajio ya kiuchumi ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/15ejr
Waziri wa fedha wa Ujerumani,Wolfgang Schäuble
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: dapd

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" lianasema tathmini iliyotolewa na shirika la kupima uwezo wa nchi wa kifedha kiuchumi, Moody's, ni tahadhari kwa Ujerumani. Shirika la Moody's limesema katika tathmini yake kuwa badala ya kuwa tengemavu, matarajio ya Ujerumani yamesimama kinyume.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine "anasema Ujerumani inapaswa kuitilia maanani tathmini hiyo. Sababu ni kwamba tofauti na tathmini zilizotolewa juu ya nchi kama Ufaransa au Marekani, shirika hilo safari hii linatimiza dhima ya mpiga mbiu-yaani linatoa tahadhari za mapema. Kwani kutokana na mgogoro wa madeni barani Ulaya Ujerumani imelemewa na mzigo mkubwa sana.

Mhariri wa "Frankfurter Allgemeine" anasema shirika hilo lina haki kabisa ya kuitahadharisha Ujerumani. Sababu ni kwamba matarajio ya maendeleo katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro kwa jumla yanaenda kinyume.

Gazeti la"Stuttgarter Nachrichten" pia linakubaliana na tahadhari iliyotolewa na Shirika la Moody's kwa kusema kwamba Ujerumani ni mtoaji fedha na pia ni mdhamini wa utengemavu wa sarafu ya Euro wakati uchumi wa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya unakwama au unashuka.Lakini uwezo wa kifedha wa Ujerumani, umevutika sana. Ndiyo sababu pia pana mashaka juu ya mdhamini mwenyewe, yaani Ujerumani.

Mhariri wa "Nordwest Zeitung" anasema tathmini ya shirika la Moody's juu ya Ujerumani ni onyo tu, si zaidi wala si pungufu ,kwani mhariri huyo anasema uchumi wa Ujerumani ni imara na unaendelea kustawi.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatoa maoni juu ya silaha za kemikali zinazomilikiwa na serikali ya Syria. Gazeti hilo linasema: "swali muhimu la kuuliza juu ya silaha hizo ni, nini kinaweza kutokea ikiwa utawala wa Assad utaanguka?

Gazeti linasema, jibu ni kwamba silaha hizo zitatoweka kama ilivyotokea nchini Iraq. Silaha hizo zinaweza kuingia katika mikono ya Hisbollah au magaidi wa Afghanistan na Irak. Lakini mhariri wa "Der Tagesspiegel " anasema silaha hizo pia zinaweza kuingia katika mikono ya waasi au maafisa wa Assad waliotamauka.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" anazungumzia wasiwasi juu ya hali inayowakabili Wakristo nchini Syria. Anaeleza kwamba pana uwezekano wa Wakristo wengi kuikimbia Syria. Watu hao wanahofia, siyo tu mabadiliko ya utawala bali pia wanahofia kwamba Wasuni watalipiza kisasi ikiwa Assad ataondoka. Kwani tayari Wakristo wameshauawa nchini Syria kutokana kuzingatiwa kuwa wanamuunga mkono Bashar al-Assad. Gazeti la "Frankfurter Rundschau" linasema nchi za magharibi zinapaswa kutumia uzito wao ili kuwalinda Wakristo wa Syria, na jamii nyingine za wachache.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Othman Miraji