1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Syria

Abdu Said Mtullya28 Agosti 2012

Pamoja na masuala mengine wahariri hao wanazungumzia juu ya mgogoro wa Syria na mkutano wa dunia juu ya maradhi ya saratani.

https://p.dw.com/p/15xwG
Mapambano yaendelea nchini Syria
Mapambano yaendelea nchini SyriaPicha: Getty Images

Mhariri wa gazeti wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" anaziangalia athari zinazotokana na mgogoro huo na hasa kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi.

Mhariri huyo anasema hasa nchi za jirani, Uturuki, Jordan na Lebanon ndizo zinazoubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi hao. Na hali imekuwa hivyo kwa miezi  kadhaa sasa. Gazeti la "Frankfurter Rundschau" linatilia maanani kwamba nchi hizo zinatumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya wakimbizi hao,na idadi yao inazidi kuongezeka kila siku. Lakini sasa nchi hizo zimefikia upeo wa uwezo wao. Ndiyo kusema  kinachohitajika sasa ni mshikamano na nchi hizo. Miito iliyotolewa na Uturuki na Jordan ya kuomba msaada kutoka nchi za magharibi bado haijajibiwa  kwa namna ya kutia moyo.

Gazeti la "Die Welt" pia linauzungumzia mgogoro wa Syria kwa kuutafakari uwezekano wa jumuiya ya kimataifa kujiingiza kijeshi katika nchi hiyo. Mhariri wa  gazeti hilo anasema ikiwa nchi za magharibi zinataka kufanikiwa kijeshi na kisiasa, kama iliyvokuwa nchini Libya na sasa nchini Syria, nchi hizo zitapaswa kuchanganya busara inayotumiwa na Uingereza na Ufaransa katika kujiingiza kijeshi barani Afrika na busara iliyotumiwa na Marekani katika eneo la Balkani yaani kusini mashariki mwa bara la Ulaya.

Katika hali hizo zote, mafanikio yalipatikana kutokana na kuweka mipaka katika harakati za kijeshi, sambamba na kuhakikisha uungaji mkono wa wananchi nyumbani.Awali ya yote ni kuepuka kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi wa nchi hizo na kuhakikisha kwamba mashambulio ya anga na misaada ya silaha kwa  wapinzani haivuki mipaka.

Harakati za kupambana maradhi ya saratani zinaendelea .Hilo ni jambo la kutia moyo. Hata hivyo mhariri wa gazeti  la "Badische Zeitung" anawataka madaktari waseme kweli. Mhariri huyo anaeleza kwamba mpaka sasa wanachofanya madaktari ni kujaribu kuyapunguza makali ya maradhi ya saratani kwa kutumia njia mbalimbali. Licha ya kusema kwamba wamo njiani kuushinda ugongwa huo,wataalamu wamearifu kwamba,bado zinatumika tiba za kuyapunguza maumivu na njia nyingine ili kuyarefusha maisha ya mgonjwa. Kwa hivyo madaktari wanapaswa kuwa wakweli kwao wenyewe , na  kwa wagonjwa wao.Kwani kinachohusika hapa siyo kusinda au kushindwa bali ni kutafuta kila uwezako uliopo  ili kuwasaidia watu wanaokumbwa na maradhi hayo.

 Gazeti la "Märkische Oderzeitung"  linatoa maoni juu ya mashindano ya michezo ya Olimpiki ya walemavu inayoanza  jijini London .Mhariri wa gazeti hilo anasema wanamichezo hao wanastahili kutiliwa maanani sawa na wanamichezo wengine.Kwa mara ya kwanza mashindano ya walemavu hao yalitangazwa moja kwa moja kutoka mjini Sidney. Lakini kabla ya hapo mashindano ya walemavu yalizingatiwa kama jambo la pembeni  tu.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Josephat Charo