Maoni ya wahariri juu ya Pistorius
21 Februari 2013Juu ya mkasa ya mkasa wa mwanamichezo maarufu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius gazeti la "Osnabrücker" linatilia maanani kwamba Pistorius anakabiliwa na mashtaka ya kumuua mpenzi wake kwa kudhamiria.Mhariri wa gazeti hilo anasema mkasa wa Pistorius unaonyesha pande mbili za maisha ya mwanadamu .
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mashtaka ya kuua kwa kudhamiria yanayomkabili Oscar Pistorius, yanaonyesha jinsi mtu ambae hadi hivi karibuni tu alikuwa nguli anavyoweza kuanguka vibaya katika maisha.Mhariri anasema ni kweli kwamba mtu hawezi kuitwa,mhalifu kabla haijathibitishwa kisheria. Lakini yaliyojitokeza kuhusu mkasa wa Pistorius mpaka sasa,yanaonyesha ukubwa wa mbwa mwitu anaeweza kujificha katika manyoya ya kondoo.
Hata hivyo mhariri wa Osnabrücker anasema,dunia inatumai kwamba kesi ya Pistorius itafanyika kwa njia za kawaida, tofauti na ile ya mwanamichezo mwengine maarufu wa Marekani O.J Simpson. Kwani waliompoteza mtoto wao wanataka haki.
Gazeti la"Junge Welt" limeandika juu ya mgogoro wa nchini Mali,baada ya serikali ya Ujerumani kuamua kuwapeleka askari wake katika nchi hiyo.
Gazeti hilo linasema Ujerumani bado ina kidonda cha rohoni,kufuatia msimamo wake juu ya harakati za kumng'oa Kanali Gadhaffi mnamo mwaka wa 2011. Ujerumani haikushiriki katika harakati hizo kinyume na nchi nyingine za magharibi.Ujerumani ilionekana kama msaliti miongoni mwa washirika wake wa magharibi.Lakini msimamo wa serikali ya Ujerumani wa wakati huo ulitokana na hisia za wananchi za kupinga vita.
Gazeti la "Junge Welt " linasema uamuzi uliopitishwa na serikali ya Ujerumani wa kuwapeleka askari, nchini Mali unaonyesha kuwa serikali hiyo sasa imesimama mbali na hisia za hapo awali za wananchi wake,aidha inadhamiria kuwa na usemi katika hali mpya ya kisiasa iliyojitokeza kaskazini mwa Afrika.
Mahakama Kuu ya Ujerumani imekiondoa kizingiti kilichokuwa kinawazuia mashoga wanaoishi pamoja,kuwaasilia watoto kwa haki sawa.Ndiyo kusema ikiwa mmoja wa mashoga amemchukua mtoto ili kumlea kama mwanawe,mwenzake pia atakuwa na haki sawa juu ya mtoto huyo.Juu ya uamuzi huo wa Mahakama kuu ya Ujerumani gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema kwa kawaida ,ndoa ni kati ya mwanamke na mwanamume.Lakini madhali ndoa za jinsia sawa nazo zinatambuliwa, basi waliofunga ndoa hizo pia wanastahiki haki zote.
Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Yusuf Saumu