Maoni ya wahariri juu ya Obama na Castro
11 Desemba 2013Mhariri wa gazeti la "Neue Westfälische" anasema kandoni mwa Ibada ya kumwombea Madiba, Rais Obama na Rais Raul Castro wa Cuba walipeana mikono. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anasema ishara hiyo ya nia njema haitaubadilisha msimamo wa Marekani juu ya vikwazo vya kiuchumi ilivyoiwekea Cuba.Lakini katika upande mwingine hatua ya Obama kumpa mkono Rais wa Cuba imeonyesha moyo wa stahamala na ubinadamu.
Jamhuri ya Afrika Kati
Gazeti la "Neue Westfälische" pia limeandika juu ya hatua ya Ufaransa ya kupeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mhariri wa gazeti hilo anasema ni wazi kwamba Rais Francois Hollande angelipendelea kuona washirika wake wakimuunga mkono kimikakati na kifedha kwa hatua aliyoichukua ya kuyapeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.Lakini anatambua kwamba huko kutakuwa sawa na kuutia mkono kizani. Washirika wa Hollande wamechoshwa na vita.
Ufaransa inazitambua hatari zinazoweza kutokea kutokana na hatua yake ya kujiingiza kijeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hatahivyo Ufaransa haina haja ya kuwa na wasi wasi mkubwa, kwa sababu waasi wa Seleka inaopambana nao siyo sawa na makundi ya wanajihadi wenye uwezo mkubwa wa kupigana.
Lakini kisiasa yapo mashaka makubwa.Ufaransa inaweza kuleta usalama wa muda tu katika Jamhuri ya Afrika ya kati lakini siyo amani na demokrasia ya kudumu.
Mgogoro wa Ukraine
Gazeti la "Sächsiche" linauzungumzia mgogoro wa nchini Ukraine na msimamo wa nchi za magharibi juu ya mgogoro huo.Mhariri wa gazeti hilo anasema nchi za magharibi zinapaswa kutambua kwamba Rais Putin ndiye alieushika mpini, wakati Ukraine imeyashika makali. Hiyo ina maana kwamba siyo lazima Putin ashiriki katika mazungumzo juu ya Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya. Yafaa kutambua kwamba watu wa nchi hiyo wamegawanyika juu ya suala hilo.Na kwa hivyo mazungumzo yataleta nini?
Naye mhariri wa "Rhein Zeitung" anasema Rais Yanukovych wa Ukraine haonyeshi dalili za kutaka kufanya mazungumzo.Anachotaka ni kupata muda zaidi.Lakini mambo yanaweza kumgeukia haraka sana. Maandamano ya wapinzani tayari yameacha athari.Na ikiwa wapinzani watabainisha kwamba Rais Yanukovych anajaribu kuwababaisha, basi watayafanya maandamano makubwa zaidi mpaka waifikie shahaba yao.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen:
Mhariri:Yusuf Saumu