Maoni ya wahariri juu ya Mshariki ya Kati na ziara ya Obama barani Asia
24 Aprili 2014Gazeti la Stuttgarter Zeitung" linazungumzia juu ya mapatano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baina ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Mhariri wa gazeti hilo anasema ni vigumu kwa nchi za magharibi kuelewa kwa nini Rais Mahmoud Abbas mwenye siasa za wastani ,ameamua kupatana na Hamas wakati ambapo mazungumzo na Israel ya kuleta amani katika Mashariki ya kati yamekaa kombo.
Hata hivyo mhariri anasema inapasa kutambua kwamba Rais Abbas anajaribu kutazama mbali.Hawezi keundelea kufanya mazungumzo na Israel kwa sababu ya kuutimiza mradi tu. Abbas anaitaka Israel iache kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina
Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter" anasema mbali na hayo, Rais Mahmoud Abbas anatambua kwamba, ikiwa mambo yataenda mrama kabisa, umoja baina ya Hamas na chama chake cha Fatah, utawapa matumaini Wapalestina wote, lakini hasa wale wa Ukanda wa Gaza.
Msimamo wa Netanyahu
Gazeti la "Weser Kurier" linauangalia msimamo wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu juu ya mapatano yaliyofikiwa baina ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.
Linasema halikuwa jambo la busara kwa Netanyahu kutoa maonyo kwa kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas na kumtaka achague kati ya Hamas na Israel. Netanyahu alipaswa kuwa na subira. Hata hiyvo anayo haki ya kuonyesha hisia zake juu ya mapatano ya Wapalestina, lakini kisiasa,amefanya kosa.
Ziara ya Obama barani Asia
Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaiuzungumzia ziara ya Rais Barack Obama katika nchi za Asia. Na linasema mataifa ya barani Asia yanaifuatilia ziara ya Obama kwa makini.Yanataka kujua ni nini hasa ataweza kukikamilisha katika ziara hiyo. Ni kweli kwamba Marekani bado ni taifa lenye nguvu kubwa kabisa duniani, kiuchumi. Lakini pia inapasa kutilia maanani kwamba uwezo wa Marekani katika kuitatua migogoro ya dunia, umepungua.
Mambo magumu kwa Umoja wa Ulaya katika Ulaya ya Mashariki
Gazeti la "Volksstimme" linatoa maoni juu ya ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika nchi za Ulaya Mashariki, Moldova na Georgia.
Gazeti hilo linaeleza kwamba mambo sasa ni magumu kwa Umoja wa Ulaya katika Ulaya ya mashariki tokea kuzuka kwa mgogoro wa Ukraine.Steinmeier na mwenzake wa Ufaransa Fabius wanafanya ziara katika nchi hizo zilizokuwamo katika himaya ya Urusi hapo awali.
Katika jimbo moja la Moldova watu walipiga kura ya maoni kuunga mkono Umoja wa forodha na Urusi ya Putin. Na kwa jumla watu wa nchi hiyo wameonyesha mashaka juu ya kuwa na uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya.Lakini licha ya ukweli huo ziara ya mawaziri hao siyo kazi bure.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo