1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mkutano wa Waislamu na serikali ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya9 Mei 2013

Wahariri wa magazeti watoa maoni juu ya mkutano baina ya wajumbe wa Waislamu na serikali ya Ujerumani uliofanyika mjini Berlin mapema wiki hii.

https://p.dw.com/p/18UkB
Waziri wa mambo ya ndani Hans-Peter Friedrich kwenye mkutano na wajumbe wa Waislamu
Waziri wa mambo ya ndani Hans-Peter Friedrich kwenye mkutano na wajumbe wa WaislamuPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano baina ya wajumbe wa Baraza la Waisalamu na serikali ya Ujerumani uliofanyika mjini Berlin mapema wiki hii umeibua hisia mbalimbali .Baadhi wanasema mikutano kama hiyo haina maana tena. Na wengine wanasema matayarisho mazuri zaidi yanahitajika. 

Gazeti la"Lausitzer Rundschau" linasema mikutano baina ya wajumbe wa Baraza la Waislamu na serikali ya Ujerumani haipaswi kuwa wasaa wa kuzungumzia juu ya hali ya hewa. Bali inapaswa kuzingatia hofu na wasiwasi wa wananchi.

Halitakuwa jambo la manufaa kufanya kana kwamba hatari inatokea upande wa kulia, tu baada ya kufichuka kwa kundi la mafashisti mamboleo la NSU.

Waziri Hans-Peter Friedrich alaumiwa:

Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anamlaumu Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Hans-Peter Friedrich kwa kutoa kauli za mashaka juu ya Uislamu na itikadi kali. Mhariri huyo anaeleza kwamba Uislamu hauzingatiwi kuwa imani ya kila siku nchini Ujerumani, licha ya kuwapo waumini Milioni nne.

Na licha ya ukweli huo, Waziri Friedrich anatoa kauli zinazoonyesha kwamba haoni  tofauti kubwa kati ya Uislamu na itikadi kali. Huo siyo msimamo wa kuwajibika, kwa  sababu unahalalisha kuongezeka chuki dhidi ya dini hiyo nchini Ujerumani.

Mhariri wa "Hannoversche Allgemeine"amekumbusha juu ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni, ulioonyesha kwamba asilimia 50 ya Wajerumani wanahisi kutishiwa na Uislamu.

Uislamu ni sehemu ya Ujerumani: 

Gazeti la "Aachener"linatilia maanani kwamba Uislamu ni sehemu ya Ujerumani na mikutano baina ya Waislamu na serikali ni muhimu. Lakini gazeti hilo linashauri  kwamba inapofanyika pasiwepo masharti yoyote.

Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" pia anasisitiza umuhimu wa mdahalo baina ya Waislamu na serikali nchini Ujerumani.Mhariri huyo anaeleza  kwamba mengi yamefikiwa katika miaka saba iliyopita.Mchakato wa utangamano baina ya wahamiaji na Wajerumani umesonga mbele. Mfano ni kutolewa kwa masomo ya dini ya kiislamu mashuleni.Na kwa hivyo mdahalo baina ya Baraza la Waislamu na serikali ya Ujerumani utapaswa uendelezwe hata baada ya kufanyika uchaguzi mkuu, lakini katika ngazi nyingine, labda chini ya uongozi wa wizara mpya ya masuala ya utangamano ikiwa itaundwa katika siku za usoni.

Mikutano yageuka kuwa mfadhaiko:

 Mhariri wa "Neue Osnabrücker "anasema mikutano baina ya Waislamu na serikali ya Ujerumani ni kazi bure! Kilichobakia baada ya miaka minane ni mfadhaiko tu. Mhariri huyo anasema kwamba mikutano hiyo sasa imefikia kiwango cha chini kabisa.

Mikutano hiyo imegeuka kuwa ya kutimiza mradi tu.Kilichobakia katika matumaini ya  mwaka wa 2006 wakati mikutano hiyo ilipoanzishwa ni mfadhaiko ,hali ya kutoaminiana na mivutano.Wajumbe wa jumuiya za Waislamu sasa wanaihudhuria mikutano hiyo kwa sababu kuonyesha heshima  tu.

Wakati Waziri wa mambo ya ndani bwana Friedrich analishikilia suala la usalama kuwa la kipaumbele kwenye mikutano hiyo, Waislamu nao wanashikilia suala la kutambuliwa kwa Uislamu kama jumuiya ya kidini nchini Ujerumani kuwa la uzito wa mbele.

Mwandishi:Mtullya  Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu