1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mkataba wa kudhibiti bajeti.

Abdu Said Mtullya30 Septemba 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya hatua mpya za kudhibiti bajeti.

https://p.dw.com/p/PQa5
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mkataba wa kudhibiti bajeti za nchi za Umoja wa Ulaya na juu ya tishio la ugaidi nchini Ujerumani.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linaipongeza tume ya Umoja wa Ulaya kwa kutangaza hatua kali dhidi ya nchi zinazoukiuka mkataba wa ustawi wa uchumi na kudhibiti bajeti.Mhariri wa gazeti hilo anasema hatua zillizotangazwa na tume hiyo zitaziimarisha taratibu zilizopo sasa za kudhibiti bajeti za nchi.

Na mhariri wa gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten anasema hatua mpya zilizotangazwa na tume ya Umoja wa Ulaya zinaonyesha kwamba tatizo siyo tu, zile nchi zisizokuwa na dhamira ya kuweka akiba bali tatizo pia ni kiwango cha chini cha ushindani cha wajasiramali wa ndani au kwa usemi mwingine nakisi katika biashara ya nje.Na ndiyo sababu, anasema mhariri huyo kwamba litakuwa jambo la manufaa ikiwa tume ya Umoja wa Ulaya itapima uwezo wa ushindani wa nchi za Umoja huo na ikiwezekana kufanya marekebisho.

Mhariri wa gazeti la Sächsiche Zeitung analizingatia suala la udhibiti wa bajeti na dhima ya vyama vya wafanyakazi kwa kusema kwamba jumuiya hizo zina haki zinaposema kwamba sasa hali ngumu inakuja kwa wananchi.

Kwa sababu serikali za nchi za Ulaya hazikukitekeleza kiapo chao wenyewe cha kuutekeleza mkataba wa ustawi wa uchumi na kudhibiti bajeti mhariri wa Sächsiche Zeitung anasema mgogoro mkubwa wa mabenki wa hivi karibuni uliufichua undumakuwili wa serikali za nchi hizo.

Gazeti la Stuttgarter linazungumzia juu ya maandamano yaliyofanyika katika nchi kadhaa za Ulaya kupinga hatua za kubana matumizi zinazochukuliwa barani Ulaya.

Gazeti hilo linasema tatizo siyo kuzisawazisha bajeti. Bali tatizo ni dhulma iliyopo katika kugawa wajibu wa kuubeba mzigo.Mgogoro wa mabenki umesababishwa na mabenki yenyewe, lakini walioubeba mzigo wa kuyaokoa mabenki hayo ni walipa kodi wa kawaida.Kwa hiyo walipa kodi hao wana haki ya kuwa na hasira

Mhariri wa Braunschweiger Zeitung leo anazungumzia juu ya tishio la mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani kufuatia taarifa iliyotolewa na mashirika ya upelelezi ya nchi za magharibi.

Mhariri huyo anasema hatari ipo,lakini haifai kuwa na kiherehere.Anaeleza kwamba katika nyakazi hizi za dunia utandawazi,Ujerumani pia inaweza kuathirika ikiwa mhubiri nchini Marekani anatangaza makusudi ya kuichoma moto Koran.

Magaidi wanachagua njia.Na Ujerumani ni nchi iliyo wazi.Na inapaswa kuendelea kuwa hivyo anatamka mhariri huyo. Kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwa macho. Lakini haipasi kuwa na kiherehere.Kwani kuonyesha kiherehere kutakuwa ushindi kwa magaidi.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Duetsche Zeitungen/

Mhariri/Josephat Charo