1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mgogoro wa Cyprus

Abdu Said Mtullya21 Machi 2013

Wahahari wanatoa maoni juu ya uamuzi wa Bunge la Cyprus wa kuupinga mpango wa Umoja wa Ulaya juu ya kukiokoa kisiwa hicho.Wahariri hao pia wanakumbusha juu ya miaka10 tokea Marekani ilipoivamia Irak.

https://p.dw.com/p/1816Y
Maandamano ya kuupinga mpango wa Umoja wa Ulaya
Maandamano ya kuupinga mpango wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters

Juu ya Cyprus gazeti la "Donaukurier "linasema sasa hali ya butaa imetanda. Gazeti hilo linaeleza kwamba ni jambo lisiloeleweka kwamba Ukanda wa sarafu ya Euro unasalimu amri mbele ya nchi ndogo. Lakini kwa kufanya hivyo nchi za sarafu ya Euro zinawanufaisha wale wenye shughuli za fedha za kizani katika kisiwa cha Cyprus. Uamuzi wa Bunge la Cyprus unaweza kuwa hatua ya kwanza kwa Cyprus kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Mhariri wa "Thüringische Landeszeitung" pia anazungumzia juu ya uamuzi wa Bunge la Cyprus kwa kutilia maanani shughuli za kifedha za kizani.

Mhariri huyo anasema hakuna mtu anaeweza kukubali fedha za walipa kodi zitumiwe ili kuziokoa fedha za kizani za Warusi zilizowekwa katika benki za Cyprus. Ikiwa mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya watasalimu amri mbele ya Cyprus,basi nchi nyingine nazo zitaufuata mfano wa nchi hiyo ndogo.Dawa ya jino bovu ni kuling'oa.

Mhariri wa "Rhein-Neckar" anasisitiza umuhimu wa kuikazia macho Cyprus. Anasema ikiwa Umoja wa Ulaya utairuhusu nchi ndogo kama Cyprus iutelekeze wajibu wake katika kuukabili mgogoro wake basi, itakuwaje kwa nchi kubwa kama Italia au Uhispania. Mambo yakiendelea hivyo, sarafu ya Euro itabakia kusomwa katika vitabu vya historia baada ya miezi michache tu na athari za kiuchumi zitakuwa kubwa kiasi cha kutoweza kupimika. Matukio ya nchini Cyprus yanathibitisha kwa mara nyingine kwamba bila ya kuwapo serikali ya Umoja wa Ulaya sarafu ya Euro itaedndlea kuwamo mashakani- na mashaka hayo yatakuwapo pia kwa Ujerumani.

Wahariri wa magazeti pia wametoa maoni yao juu ya Iraq. Watu wa nchi hiyo wanakumbuka mwaka wa kumi tokea Marekani ilipoivamia nchi yao.

Mhariri wa gazeti la "Mittelbayarische Zeitung" anasema raia zaidi ya laki moja waliuawa. Askari wa Marekani alfu nne na mia nane pia waliuawa na maalfu wengine walijeruhiwa.Kuangushwa kwa Saddam Hussein siyo hatua iliyoleta matumaini kwa watu wa Irak.Kwa jumla Iraq siyo nchi inayoweza kutumiwa na Marekani kama mfano mzuri, badala yake nchi hiyo ni mshirika wa Iran.

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deuetsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman