1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Mfalme Willem-Alexander

Abdu Said Mtullya30 Aprili 2013

Uholanzi imepata Mfalme, Willem -Alexander. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao. Pia wanazungumzia juu ya mvutano baina ya Ujerumani na Ufaransa

https://p.dw.com/p/18PW7
Sherehe za Mfalme Willem Alexander kuvikwa taji
Sherehe za Mfalme Willem Alexander kuvikwa tajiPicha: PATRIK STOLLARZ/AFP/Getty Images

Mhariri wa "Nordkurier "anasema Mfalme Willem Alexander amevikwa taji baada ya Malkia Beatrix kujiweka kando. Mhariri wa "NordKurier"anaeleza kuwa Malkia Beatrix aliamua kujiuzulu baada ya kuzisoma alama za nyakati.Alitambua kwamba wakati wake ulishapita wa kulivaa taji.

Mhariri wa gazeti la "Nordkurier"anasema Malkia Beatrix alitambua kwamba mwanawe,Willem Alexander, yupo karibu zaidi na wananchi kuliko yeye. Hali hiyo inamletea heshima kubwa miongoni mwa wananchi hao.

Naye mhariri wa gazeti la "Frankfurter Neue Presse" anasema Mfalme Willem-Alexander anaewakilisha rika la usasa anapaswa kuwa tofauti na wazazi wake. Mhariri huyo anasema ni wazi kwamba Mfalme Willem Alexander hana haja ya kujithibitisha. Anajulikana. Lakini kama mrithi wa ufalme wa rika la leo anapaswa kuwa tofauti na wazazi wake.Kwa mfano anapaswa kuwa na ufahamu mkubwa wa mambo ya soko na matumizi bora ya fedha, badala ya kuishi katika enzi za paukwa pakawa.

Gazeti la "Westfälische Nachrichten"linazungumzia juu ya mvutano baina ya Ujerumani na Ufaransa kuhusu sera ya kubana matumizi. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasisitiza umuhimu wa uhusiano baina ya nchi mbili hizo katika Umoja wa Ulaya.Anaeleza kwamba uwezekano wa Rais Hollande kuleta mageuzi unazidi kuwa finyu,licha ya ukweli kwamba yeye pia unautambua umuhimu wa mageuzi hayo. Mgororo wa madeni unaweza kutatuliwa kwa juhudi za pamoja tu.

Urafiki baina ya Ujerumani na Ufaransa haukuwa tu msingi wa kuleta Umoja wa Ulaya bali pia leo ndiyo nguzo inayoishikilia sarafu ya Euro. Bila ya Ufaransa, Ujerumani itasimama peke yake. Ni kweli kwamba ,siyo rahisi kwa marafiki kupatana wakati wote, lakini inafaa kujaribu.

Mhariri wa "Nordwest" anasema njia ambayo Rais Hollande anaitumia ili kuyafunikiza matatizo yake ni ya kizamani. Lakini njia hiyo pia ni ya hatari.

Mhariri huyo anaeleza kwamba mambo yanaenda mrama kwa Rais Hollande na watu wake. Anautumia ujanja wa enzi za kale kwamba iwapo mtu ameshindwa kutilimiza jambo fulani basi amtafute mtu wa kumsingizia.Hiyo kwa kweli ni njia ya hatari. Serikali ya wasoshalisti nchini Ufaransa inafanya makosa kwa kuchochea hisia dhidi ya Ujerumani. Na hayo yote yanatokana na mtazamo wa kupinga sera za kubana matumizi. Rais Hollande anapaswa kutambua kwamba kutokana na kuwa imara, Ujerumani kwa sasa inaibeba pia Ufaransa.

Mwandishi:Mtullya abdu./Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Gakuba Daniel