1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mapigano baina ya Israel na Hisbollah

Abdu Said Mtullya29 Januari 2015

Wahariri wa magazeti katika safu zao za maoni wanazungumzia juu ya mkasa ulitokea kwenye mpaka wa Israel na Lebanon na juu ya kuanza kusambaratika kwa Pegida baada ya viongozi kadhaa wa kundi hilo kujiuzulu

https://p.dw.com/p/1ESYc
Askari wa Israel kwenye mpaka na Lebanon
Askari wa Israel kwenye mpaka na LebanonPicha: Reuters/B. Ratner

Gazeti la "Der neue Tag"linazungumzia juu ya mapambano yaliyotokea baina ya wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Hisbollah. Askari wawili wa Israel waliuawa katika mapigano hayo, na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Juu ya kadhia hiyo mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anakumbusha kwamba hii si mara ya kwanza kutokea mkasa kama huo ambao baadae ulisababisha moto mkubwa zaidi. Hata hivyo hakuna anaetaka kuyaona tena yale yaliyotokea miaka tisa iliyopita, wakati ambapo majeshi ya Israel yaliivamia Lebanon ili kuwafuatilia wapiganaji wa Hisbollah.

Naye mhariri wa gazeti la "die tageszeitung" anasema ilikuwa wazi kwamba Hisbollah watalipiza kisasi baada ya kamanda wao kuuliwa na Israel katika shambulio la ndege. Mhariri huyo anasema kadhia ya jana inaonyesha jinsi mipaka ilivyokuwamo katika hali ya mvutano katika Mashariki ya Kati.

Pegida yaanza kusambaratika?

Gazeti la "Süddeutsche" linatoa maoni juu ya kujiuzulu kwa viongozi kadhaa wa kundi la Pegida la watu wanaopinga kuenezwa Uislamu barani Ulaya Gazeti hilo linasema kilichokuwa kinawaleta pamoja viongozi hao kilipoteza mashiko siku nyingi. Baada ya kujiuzulu kiongozi wa hapo awali wamefuatia wengine.

Katika kipindi kifupi tu kundi hilo limewapoteza viongozi wake muhimu. Hata hivyo haitakuwa sahihi kabisa kuanza kuzungumzia juu ya mwanzo wa kusambaratika kwa kundi hilo la Pegida. Wale wanaowachukia wageni wataendelea kuipeleka chuki yao barabarani.

Serikali mpya hatua mpya, Ugiriki
Serikali mpya ya Ugiriki imezitangaza hatua za kwanza inazokusudia kuzichukua, ikiwa pamoja na kuusimamisha mchakato wa kuzibinafsisha mali za taifa.

Gazeti la "Tagesspiegel" linasema ,Waziri Mkuu wa Ugiriki,Tsipras anazungumzia juu ya kuusimamisha mpango wa kuzibinafsisha mali za taifa,pia anazungumzia juu ya kuwarudisha kazini maalfu ya watumishi wa umma walioachishwa kazi hapo awali na pia amezungumzia juu ya kuubatilisha mkataba wa vitega uchumi uliokwishatiwa saini baina ya Ugiriki na kampuni moja ya China Cosco.

Gazeti la "Tagesspiegel " linasema kwa hatua hizo serikali mpya ya Ugiriki inatoa ishara mbaya sana kwa wawekaji vitega uchumi kutoka nje. Na sasa siyo jambo la ajabu kwamba soko la hisa la Ugiriki limeanguka.

Gazeti la "Berliner" linatoa maoni juu ya mtazamo wa serikali mpya ya Ugiriki kuhusu mgogoro wa nchini Ukraine. Mpaka sasa nchi za Umoja wa Ulaya zimesimama pamoja dhidi ya Urusi kuhusiana namgogoro huo. Lakini sasa serikali mpya ya Ugiriki imevilaumu vitisho vya Umoja wa Ulaya vya kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

Gazeti la "Berliner" linasema inapasa iwe wazi kwa Ugiriki kwamba lengo ni kuiambia Urusi kwamba inauvuruga utaratibu wa mipaka barani Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Duetsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu