1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wataka kubadilisha sheria ya uhamiaji

Admin.WagnerD7 Aprili 2016

Wahariri wanazungumzia juu ya mageuzi ya sheria inayohusu hifadhi ya ukimbizi katika nchi za Umoja wa Ulaya na pia wanatoa maoni juu ya sheria ya kupiga marufuku ukahaba wa kulazimisha.

https://p.dw.com/p/1IRKU
Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya
Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters/F. Lenoir

Gazeti la "Rheinpfalz" linasema pendekezo la kuibadilisha sheria ya hifadhi ya ukimbizi katika nchi za Umoja wa Ulaya ni wazo zuri lakini Utekelezaji wake utakuwa mgumu bila ya ridhaa ya wote.

Mhariri wa gazeti hilo anasema sheria inayotumika sasa haitoi haki sawa kwa wanachama wote wa Umoja wa Ulaya. Na kwa hivyo anaeleza kinachopasa kufanyika ni kuibadilisha kabisa sheria hiyo badala ya kuifanyia ukarabati tu!

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema mkataba wa Dublin unaoweka msingi taratibu za hifadhi ya ukimbizi barani Ulaya, una mapungufu kwa sababu unaziwezesha nchi fulani kuukwepa wajibu.

Hatahivyo mhariri wa gazeti la " Der neue Tag" anasema mageuzi yanayozungumziwa juu ya sheria ya hifadhi ya ukimbizi ni paukwa pakawa tupu. Mhariri huyo anaeleza kwamba pendekezo juu ya kuleta haki katika kuutimiza wajibu juu ya wakimbizi miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya ni hadithi tu. Sababu ni kwamba hakuna mshikamano miongoni mwa nchi wanachama.

Gazeti linasema bara la Ulaya siyo tu mahala pa hifadhi kwa watu wanaoandamwa kisiasa. Bali Ulaya ni eneo la uhamiaji linalokabiliwa na shinikizo kubwa na kutokana na ukweli huo, pendekezo juu ya kuifanyia mageuzi sheria ya hifadhi ya ukimbizi ni porojo tu.

Ukahaba wa kulazimisha

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linatoa maoni juu ya sheria ya kupiga marufuku ukahaba wa kulazimisha nchini Ujerumani.Mhariri wa gazeti hilo anasema uhalifu huo lazima upigwe vita. Lakini anaeleza kwamba hiyo siyo kazi rahisi.

Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas
Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Mhariri wa gazeti hilo anasema iwapo lengo la kupiga marufuku ukahaba wa kulazimisha litafikiwa, inategemea na juhudi za wanasiasa, mashirika ya kutetea haki za akina mama na asasi nyingine za kijamii.

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" anahoji kwamba hata ikiwa sheria mpya itapitishwa uhalifu wa ukahaba wa kulazimisha bado utaendelea kuwepo.

Kinachotakiwa anasema mhariri wa gazeti hilo ni kuushughulikia mzizi wa tatizo.

Mswada wa sheria mpya juu ya kupiga marufuku ukahaba wa kulazimisha, umesimama mbali sana na hali halisi.

Gazeti la "Berliner Zeitung" linazungumzia juu ya kinyang'anyiro cha wagombea tiketi ya kukiwakilisha chama cha Demokratik katika uchaguzi wa Rais nchini Marekani.

Mhariri huyo anasema kwamba mjumbe anaepewa nafasi kubwa zaidi, Hillary Clinton bado hajakuwa na uhakika wa kuibeba bendera ya chama chake. Mshindani wake Bernie Sanders anawavutia sana vijana.

Hayo yameonekana Wisconsin ambako Sanders alishinda vizuri.

Mhariri wa "Berliner Zeitung " anasema Hillary Clinton aliewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, ameingiwa wasi wasi baada ya kipigo cha Wisconsin.

Mwandishi:Mtullya abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga