Maoni ya wahariri juu ya kudakizwa mawasiliano ya simu na mtandao nchini Marekani
10 Juni 2013Gazeti la"Landeszeitung" linakumbusha kauli ya hapo awali, kwamba mawasiliano ya mtandao wa internet yanapaswa kuwa njia ya mawasiliano bila ya kuwapo vipingamizi vyovyote. Lakini sasa njia hiyo imegeuzwa kuwa chombo cha upelelezi na shirika la ujasusi la Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anasema kufichuliwa kwa kashfa hiyo kunathibitisha kwamba, njia ya kuelekea katika nchi ambamo watu wanamulikwa kikamilifu na mashirika ya ujasusi ni fupi sana.
Naye mhariri wa gazeti la "Hamburger Abendblatt" anasema kashfa hiyo inalichafua jina la Rais Obama,ambae ni mshindi wa nishani ya amani ya Nobel .
Mhariri huyo anealeza kwamba hakuna sababu inayoweza kuhalalisha upelelezi wa kiwango hicho, ya kuutegesha mtandao wa dunia nzima kwa lengo la kuyadukua mawasiliano ya jamii nzima. Kwani mtandao huo unasadia nini? Mbona Marekani haikuweza kuyaepusha mashambulio ya Boston na wala Marekani haijaweza kuufanya usalama wa askari wake nchini Afghanistan kuwa mkubwa zaidi?
Mkutano wa kilele wa Obama na Xi Jinping:
Gazeti la" Berliner Zeitung" linauzingatia mkutano wa siku mbili wa Marais, Xi Jinping na Barack Obama uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.Mhariri wa gazeti hilo anasema Marekani na China si marafiki wala maadui .Lakini kiuchumi nchi hizo zinategemeana.Hali hiyo inaufanya uhusiabo baina yao uwe mgumu. Ndiyo sababu kauli zilizotolewa na Marais Obama na Xi Jinping juu ya mazungumzo yao zinapaswa kutiliwa maanani.
Wote wametoa mwito wa kuwepo ruwaza mpya ya ushirikiano baina ya nchi zao.Katika muktadha wa mazingira magumu, yaliyopo baina ya Marekani na China mwito huo wa kuanzisha muundo mpya wa ushirikiano, ni hatua muhimu sana.
Ujerumani bado imekukmbwa na mafuriko :
Gazeti la "Volksstimme" linatoa maoni juu ya maafa ya mafuriko yaliyozikumba sehemu kadhaa za Ujerumani. Mhariri wa gazeti hilo anasema hadi,sasa takwimu nyingi na historia ndefu zimetolewa juu ya mafuriko hayo.Lakini kinachotakiwa kutolewa zaidi, sasa ni msaada.
Naye mhariri wa "Hannoversche Allgemeine" anasisitiza kwa kusema kwamba wanasiasa hawatasaidia kwa kukumbusha juu ya maafa yaliyotokea katika karne iliyopita. Mafuriko hayana msalie na hali ya hewa haitabadilishwa kwa kutoa takwimu.Maafa hayo yamethibitisha kwa mara nyingine kwamba waokoaji na watoaji fedha wataendelea kuhitajika.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Abdul-Rahman