Maoni ya wahariri juu ya Iraq na Ukraine
26 Juni 2014Juu ya Iraq ya gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger linaziangalia athari za vita vya nchini humo Iraq kwa WaKurdi. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba jamii ya Wakurdi wanaofikia Milioni 40 kwa jumla nchini Iraq na Uturuki ndiyo jamii pekee kubwa ya watu wasiyokuwa na nchi yao. Lakini matukio ya nchini Iraq sasa yanaisogeza karibu ndoto ya watu hao ya kuwa na nchi yao. Na hakika kuwapo kwa nchi imara ya Wakurdi kutaleta manufaa pia kwa Uturuki.
Mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger"anasema wakaiti sasa umefika kwa Wakurdi kuwa na nchi yao. Jee Uturuki nayo ipo tayari kusaidia?
NATO katika mtanziko
Gazeti la "Saarbrucker" linauzungumzia mvutano baina ya mfungamano wa kijeshi wa NATO na Urusi. Gazeti hilo linasema Nato inakabiliwa na mtanziko.Mhariri wa "Saarbrücker"anaeleza kwamba sasa inazidi kuwa dhahiri miongoni mwa nchi za NATO kwamba katika mgogoro wa Ukraine,Rais Wladimir Putin amezidi kete.Putin anatumia kauli za undumakuwili na ahadi za udanganyifu ili kuitekeleza sera yake juu ya Ukraine. Sasa wanachama wa NATO wanavutana wenyewe na wamenasa katika mtego wa kuzirudia kali zao dhidi ya Urusi.Nato imekwama.
Mhariri wa gazeti la "Nürnberger" anasema watu wa mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitenga hawajui kwamba wanatumiwa kama chambo na Rais Putin. Na utakapofika wakati wa kuwatelekeza atafanya hivyo baada ya kuifikia shabaha yake nchini Ukraine.
Ujerumani ishiriki kijeshi nje
Kauli ya Rais wa Ujerumani Joachim Gauck juu ya kuitaka Ujerumani ishiriki zaidi katika kuitatua migogoro ya kimataifa,pia kijeshi, imezua mjadala miongoni mwa wabunge wa Ujerumani .Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linatoa maoni kwa kusema kwamba ni wazi kwamba inaruhusiwa kumkosoa Rais wa Ujerumani anapozungumza kana kwamba jukumu kuu la Ujerumani katika nchi za nje ni la kijeshi tu. Hata hivyo yeyote anaejaribu kumwita Rais huyo kuwa mchochezi wa vita, basi mtu huyo hailewei thamani ya demokrasia.
Udereva bila ya leseni
Jee ni adhabu gani inayostahili kutolewa kwa watu wanaoendesha magari bila ya kuwa na leseni za udereva? Gazeti la "Eisenacher Presse" linasema watu wanaoziona fedha zao kuwa tamu kiasi cha kutenda uhalifu wa kuendesha magari bila ya leseni, wanastahili kupewa adhabu ya kulipa faini kubwa.Wakilipa fedha, wataguswa pale ambapo hasa panawauma.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman