1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafanikio ya Obama

16 Julai 2015

Katika tahariri zao wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya mafanikio yanayotokana na mazungumzo ya Vienna juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.Pia wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Ugiriki.

https://p.dw.com/p/1FzvF
Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Getty Images/A. Wong

Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linayazungumzia makubaliano yaliyofikiwa na Iran kwa kuziangalia juhudi zilizofanywa na Rais Barack Obama.

Mhariri wa gazeti hilo anasema Rais Obama anaendesha siasa kama sanaa ya kufanya kile kinachowezekana, na katika hilo amepata mafanikio makubwa. Mhariri wa "Flensburger Tageblatt" anatilia maanani kwamba Obama aliuokoa uchumi wa Marekani baada ya kutokea mgogoro wa mabenki.

Mhariri anasema Obama pia amefanikiwa kuleta mageuzi katika mfumo wa afya nchini Marekani na alifanikiwa kumfagilia mbali gaidi Osama bin Laden. Na kutokana na makubuliano yaliyofikiwa na Iran Obama ameuthibitisha msemo wake " Yes We Can" Ndiyo tunaweza.

Gazeti la "Der neue Tag" linasema makubaliano yaliyofikiwa baina ya Iran na jumuiya ya kimataifa ni hatua ya kihistoria.Mhariri wa gazeti hilo anasema mkataba uliofikiwa ni fursa ya pekee ya kuanza mambo upya.

Usalama zaidi katika Mashariki ya Kati

Mhariri wa "Der neue Tag" anasema mkataba uliofikiwa na Iran utatoa mchango katika kulifanya eneo la Mashariki ya Kati liwe la usalama zaidi ambalo vinginevyo linakabiliwa na migogoro chungutele ya umwagikaji wa damu. Na kwa watu wa Iran wenyewe anasema mhariri huyo, mkataba uliofikiwa juu ya mpango wake wa nyuklia, ni ahadi ya kuwaletea neema.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hakubaliani na mkataba uliofikiwa na Iran. Gazeti la "Braunschweiger" linasema Waziri Mkuu Netanyahu ametangaza vita dhidi ya mkataba huo. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba bwana Netanyahu anaungwa mkono na mwanasiasa wa upande wa upinzani alisema kuwa Iran inadanganya.

Mwanasiasa huyo, anasema mhariri wa gazeti la "Braunschweiger, ameisuta Iran kwa kuongopa juu ya vituo vyake vya kinyuklia ambavyo, maafisa wa Umoja wa Mataifa hawakuweza kuvikagua bila ya kuomba ruhusa, siku 24 mapema.

Ugiriki bado ni tatizo katika umoja wa sarafu ya Euro

Gazeti la "Rhein-Necker" linauzungumzia mgogoro wa madeni katika Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba katika Umoja huo ziko njia mbili, lakini moja ni ile ya mwendo wa kasi zaidi inayotumiwa na Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.

Mhariri wa "Braunschweiger anasema Waziri Schäuble hana subira. Na kwa hivyo, anasema mhariri huyo, siyo jambo la ajabu kuamini kwamba waziri huyo anaunga mkono kufukuzwa kwa Ugiriki kutoka kwenye sarafu ya Euro.Lakini mhariri wa "Brauschweiger" anaeleza kuwa Schäuble anaiwakilisha hofu ya watu wengi barani Ulaya.

Mhariri wa gazeti la "Aachener" anatoa maoni juu ya hukumu iliyotolewa kwa aliekuwa mlinzi kwenye kambi ya mafashisti wakati wa vita vikuu vya pili.

Mhariri wa gazeti hilo anasema hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya mji wa Lüneburg kwa mhalifu mwenye umri wa miaka 94 siyo ya mwisho. Anasema bado wapo wahalifu,ambao wengi wao wameshavuka umri wa miaka 90,ambao hawajafikishwa mbele ya sheria. Mhariri anasema kuwasaka na kuwakamata wahalifu hao ni jukumu la wanasheria.

Lakini jambo muhimu anasema mhariri wa gazeti la "Aachener" ni kuhakikisha kwamba wahalifu hao hawapati mahala pa kujificha!

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo