Maoni ya wahariri juu ya hali ya Iraq
17 Juni 2014Juu ya mgogoro wa Iraq gazeti la "Reutlinger General Anzeiger" linayatilia maanani mazungumzo baina ya Marekani na Iran. Mhariri wa gazeti hilo anasema litakuwa shauri jema ikiwa nchi za magharibi zitaihusisha Iran katika juhudi za kuyatafuta masuluhisho ya matatizo ya Mashariki ya Kati na nchi zote zinazopakana na eneo hilo.Ni kweli kwamba Iran inawafadhili Hisbollah, lakini Saudi Arabia pia inawafadhili Wasuni wenye itikadi kali duniani kote.Na kwa hivyo Marekani inapaswa ishirikiane na Iran .
Urusi yaifungia bomba Ukraine
Wahariri leo pia wanatoa maoni yao juu ya mgogoro wa gesi baina ya Urusi na Ukraine, unaoweza kuziathiri nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya. Gazeti la "Der neue Tag"linasema mkakati wa Rais Putin juu ya Ukraine uko wazi kabisa.Baada ya kuiyumbisha nchi hiyo kisiasa,kijeshi na kijamii sasa Urusi inalenga shabaha ya kuiyumbisha Ukraine kiuchumi. Kwa kipindi cha muda mrefu mkakati huo wa kuishinikiza Ukraine utaziathiri Ujerumani na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.
Naye mhariri wa "Saarbrücker" anasema hakuna mtu alietarajia kwamba mzozo wa gesi baina ya Urusi na Ukraine ungelitatuliwa kwenye meza ya mazungumzo. Ndiyo kusema kwamba mvutano wa kisiasa bado unaendelea.Sasa Urusi inaiendeleza kampeni yake dhidi ya Ukraine kwa kutumia njia nyingine.Na gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema hatimaye ni walipa kodi katika nchi za magharibi watakaolibeba zigo.Gharama za kuiwezesha Ukraine iondokane na nira ya Urusi,zitakuwa kubwa.
Ujerumani kushiriki kijeshi nje ya nchi
Gazeti la "Rhein -Necker " linaizungumzia kauli ya Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck juu ya sera ya nje ya Ujerumani. Bwana Gauck amesema Ujerumani inapaswa ishiriki zaidi katika kuwasaidia wale wanaokandamizwa duniani.
Juu ya kauli hiyo, mhariri wa gazeti la "Rhein Necker" kwanza anauliza jee hao wanaokandamizwa ni watu gani?Rais Gauck anafanya makosa kwa kujiingiza katika masuala ya kisiasa. Labda serikali inapendezwa na mtazamo huo lakini kwa kweli anachofanya Rais huyo siyo jambo la busara.
Naye mhariri wa "Tagespiegel" anasema Ujerumani sasa imo katika mchakato wa kuyapitisha maamuzi ya kimsingi. Ni kweli inashiriki katika juhudi za kuyatatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi duniani.Lakini inapohusu kushiriki katika juhudi za kijeshi,wanasiasa wanaogopa kupitisha maamuzi kwa sababu ya kuhofia kuwakasirisha wapiga kura wao. Lakini kwa kufanya hivyo wanaifanya Ujerumani ipoteze imani miongoni mwa washirika wake wa Umoja wa Ulaya na wa Nato.
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman