1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Baba Mtakatifu

Abdu Said Mtullya29 Machi 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia ziara ya Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 inayomalizika katika kisiwa cha Cuba. Wanasema angeliweza kufanya zaidi kwa ajili ya wapinzani.

https://p.dw.com/p/14Urm
Papa Benedikt wa 16 akiongoza misa Havanna
Papa Benedikt wa16 akiongoza misa HavannaPicha: Reuters

Mhariri wa "Berliner Zeitung" anasema katika ziara zake za Mexico na Cuba, Baba Mtakatifu alizizingatia kanuni za kanisa na kupuuza hali halisi.Alifanya mazungumzo na Marais waliopo madarakani, Marais wa zamani na viongozi wa makanisa. Gazeti la "Berliner Zeitung"linatilia maanani kwamba wawakilishi wa makundi yaliyopo kandoni mwa jamii walibakia nje ya mazungumzo hayo. Wapinzani kisiwani Cuba wangelipata moyo endapo angelitoa kauli juu ya mazingira yanayowakabili.

Mhariri wa gazeti la "Nordbayerischer Kurier" anasema Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 amesimama njia panda. Katika upande mmoja ameyazungumzia yaliyopaswa kuzungumziwa, lakini katika upande mwingine alitumia mateke ya kuku juu ya masuala fulani. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kuwa ,kwa Baba Mtakatifu ziara ya Cuba ni zoezi la kidiplomasia ya nadhari kubwa.

Katika upande mmoja Benedikt wa 16 angeliweza kutoa kauli za uwazi juu ya masuala ya haki za binadamu kisiwani Cuba. Lakini katika upande mwingine alikuwa mwangalifu sana katika matamshi yake. Hayo yanatokana na mtanziko unaolikabili kanisa kisiwani Cuba. Kanisa katoliki kisiwani Cuba linaamini kwamba diplomasia itasaidia kuleta mabadiliko. Na ndiyo sababu linawakumbatia wenye mamlaka.

Mhariri wa"Nordbayerischer Kurier" anakumbusha katika maoni yake kwamba Kadinali wa Havana aliwaita polisi wakati wapinzani walipolikalia kanisa, kabla ya ziara ya Baba Mtakatifu kuanza. Yumkini lengo la Kadinali huyo ni kuepusha mvutano na idara za serikali. Analoweza kulisema mtu kwa sasa ,ni "haleluya" na kutumai kwamba mambo yatabadilika kisiwani Cuba.

Naye mhariri wa "Frankfurter Allgemeine" anasema ziara ya Baba Mtakatifu ilikuwa na manufaa kwa watawala wa Cuba. Mhariri huyo anaeleza kwamba wapinzani wa Cuba walipaswa kuyasikia maneno ya kuwatia moyo kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani,sembuse kukutana na wapinzani hao. Alipozungumzia juu ya haki za binadamu Baba Mtakatifu aliishia katika mawanda ya uhuru wa kuabudu tu. Na kwa hivyo ikiwa lengo la mazungumzo yake na Rais Raul Castro liliishia katika kumshawishi, Rais huyo ili Ijumaa kuu iwe siku kuu kisheria katika kisiwa cha Cuba basi, ziara yake ilikuwa ya mafanikio kwa utawala wa wakomunisti.

Mhariri wa "Nordwest" anasema kuwa ziara ya Baba Mtakatifu kisiwani Cuba imeacha alama kubwa ya kuulizaJee ziara hiyo itauathiri ukomunisti? Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 aliwakumbusha watu juu ya haki ya binadamu kuwa huru. Mwenzake John Paul wa Pili alitoa ujumbe kama huo miaka 30 iliyopita nchini Poland. Na kwa ujumbe huo aliufungua ukurasa mpya wa historia.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef