XI Jinping ajiimarisha zaidi mamlakani
17 Oktoba 2022Haijawahi kutokea mkutano wa chama cha Kikomunisti cha China kuwa na maswali mengi yasio na majibu kuhusu mwelekeo wake na watumishi kama ilivyo kwenye mkutano wa sasa ulioanza Jumapili. Hata kama ni dhahiri kwamba nahodha atabakia kuwa yule, hakuna ajuaye bado nani watakuwa marubani katika uongozi wa pamoja wa chama cha CP.
Mabadiliko ya kizazi katika uongozi wa chama yamekuwa ya kutabirika na kuaminika katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, kwa sababu wakati wote kulikuwa na makada wawili wenye umri wa miaka 55 kwenye kamati ya kisiasa ya chama, ambayo ndiyo inayoshikilia madaraka. Xi Jinping mwenyewe alifanikiwa kukaa kwenye kamati hiyo kwa njia hiyo mwaka 2007. Alikuwa na umri wa miaka 54 wakati huo.
Lakini kwenye mkutano wa mwisho miaka mitano iliyopita, hakuingiza wanasiasa wa namna hiyo kwenye kamati ya kisiasa ya chama. Xi mwenye umri wa miaka 69 hivi sasa anatarajiwa kuwania muhula wa tatu, ingawa kwa mujibu wa sheria zisizo rasmi za chama anapaswa kustafu baada ya kutimiza umri wa miaka 68. Wakati wa mihula yake mwili alishinikiza sheria za chama zibadilishwe kwa namna inayomfaa yeye na kuifanyia marekebisho katiba.
Kwa njia hii aliwezesha pia muhula wa tatu kwa ofisi yake nyingine kama Rais. Hatua hizo haziachi mashaka yoyote kwamba Xi anataka kuendelea kuitawala China kama kiongozi wa chama na taifa ambaye anaongoza pia vikosi vyote vya jeshi la China. Ili kupata uongozi kamili, wanachama wenzake wamepandishwa vyeo na waoweza kuwa wapinzani wameondolewa njiani.
Ndani ya chama na hata miongoni mwa umma, Xi amechukuliwa kwa muda mrefu kuwa mwanasiasa mwenye nguvu zaidi katika historia ya China. Madaraka nchini humo hayajawahi kulimbikiziwa kwa mtu mmoja, siyo hata wakati mwasisi wa taifa hilo Mao Zedong alipoitawala China. Siyo chama cha CP pekee kinachokabiliwa na mabadiliko muhimu ya mwelekeo.
Mwelekeo wa zamani, changamoto mpya
Taifa hilo la chama kimoja linakabiliwa na changamoto nyingi. Kwanza kabisaa ni janga la corona ambalo limetatiza maisha ya umma katika miji mikubwa ya China na hivyo kupunguza kasi ya ukuaji. Sera ya kuwa na mambukizo sifuri ya covid katika taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya watu duniani ina changamoto zake pia.
Soma pia: Rais Xi apongeza utawala wa chama cha Kikomunisti
Taifa hilo limejitenga na ulimwengu kupitia vizuwizi vikali vya kuingia, lakini pia ndani ya nchi kwenyewe, sera hiyo haijaweza kuzuwia mambukizi. Hii inafanya kurejea kwa China katika jumiya ya kimataifa kuwa changamoto ya muda, hata miaka kadhaa baada ya kuzuka kwa janga hilo.
Hakuna anayethubutu kutoka nje ya kifuniko
Wanaharakati wa haki za binadamu pia wanahofia kuongezeka kwa ukandamizaji na kiongozi mpya wa zamani wa chama. Xi amedhirisha kwamba anahalisha mamlaka kupitia mfumo kandamizi wa utawala na propaganda iliyojazwa itikadi.
Kwa mfano, inapokuja kwenye masuala kama jamii ya wachache ya Waislamu wa Uyghur, Taiwan ambayo Beijing inaoiona kama jimbo lililojitenga, na mji wenye mamlaka yake ya ndani wa Hong Kong, anatumia ubabe na kufanya ukandamizaji wa kikatili ili kujionesha kama mtu mwenye nguvu. Haki za kiraia zinadhibitiwa, na wakosoaji wa utawala wanafungwa.
Hata ndani ya chama, mtindo huu wa uongozi unaangaliwa kwa utata katika makundi mbalimbali, waangalizi wanaamini. Hakuna anaethubutu kumpinga Xi Jinping chini ya mazingira ya sasa. Wagombea wa nafasi za kamati ya siasa wanasalia kuwa kimya kama panya siku hizi.
Soma pia: Namna Xi Jinping alivyojilimbikizia madaraka katika muongo mmoja
Yeyote anaefanya kosa dogo tu hupoteza kinyanganyiro kabla ya kufika mwisho. Na sasa ni wakati kwa kila mmoja kula kiapo cha utiifu wa milele kwa kiongozi wa chama kabla ya maamuzi haya muhimu kuhusu viongozi.
Ni kweli kwamba sera ya kigeni na kiuchumi hazitakuwa kipaumbele cha mkutano huu. Lakini angalau dunia inaweza kuona ishara na namna China itaongozwa katika miaka ijayo kutokana na muundo wa uongozi wake.
Kamati ya kudumu itaundwa na kutambulishwa kwa umma katika siku ya mwisho ya mkutano. Mkutano wa chama kawaida hudumu kwa kati ya siku tano hadi saba. Haijalishi watu gani watasimama kwenye zulia jekundu, wana jambo moja la kufanana: Xi na marafiki zake wanatawala tena.