1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Zarif ajiuzulu

Oumilkheir Hamidou
26 Februari 2019

Uamuzi wa kujiuzulu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Zarif unadhihirisha jinsi siasa shupavu ya Marekani inavyoleta mabadiliko Teheran-Wafuasai wa siasa kali wanapata nguvu

https://p.dw.com/p/3E7mk
Deutschland München MSC Mohammed Dschawad Sarif
Picha: Reuters/A. Gebert

Uamuzi wa kujiuzulu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Jawad Zarif ni ishara. Mamoja kama rais Hassan Rohani ataukubali au la. Ni uamuzi wa mwanasiasa wa Iran, Zarif, ambae hakuna kama yeye anaefungamanishwa zaidi na mkataba wa nuklea wa Iran. Mtu aliyesomea Marekani na kuishi miongo kadhaa huko na aliyetaka kufungua milango ya nchi hiyo.

Mkataba unaojulikana kwa jina Joint Comprehensive Plan of Action kwa kifupi JCPoA ulipofikiwa mwaka 2015, watu walishangiria majiani nchini Iran. Wahafidhina hawakufurahiswa si na makubaliano yaliyofikiwa na wala si na jinsi wananchi walivyoteremka majiani kwa ghafla kushangiria wakipa matumaini.

Ngoma ya Tari iliyofuatiwa na mikataba ya silaha

Mhariri wa DW, Matthias von Hein
Mhariri wa DW, Matthias von Hein

Matokeo ya makubaliano hayo wananchi hawajakawia kuyashuhudia: shughuli za kiuchumi ziliimarika, sekta ya utamaduni na utalii zikinawiri. Hata kama tija halisi ya makubaliano hayo haikufikia matarajio. Upepo wa mageuzi ulipelekea mfuasi wa siasa ya wastani Hassan Rohani kuchaguliwa tena uchaguzi wa rais ulipoitishwa mwaka 2017. Watu wakateremka upya majiani kusherehekea huku rais mpya wa Marekani Donald Trump akifanya ziara yake ya kwanza ughaibuni kwa kuitembelea Saudi Arabia. Akimulikwa na kamera za dunia alishika upanga na kucheza tari. Ngoma hiyo imefuatiwa na mikataba chungu nzima ya biashara ya silaha kwa nchi hiyo ya kifalme tajiri kwa mafuta.

Uamuzi wa upande mmoja wa kujitoa Marekani katika makubaliano yanayodhaminiwa na sheria za kimataifa kuhusu mradi wa nuklea ukawapa haki wale ambao mjini Teheran wamekuwa wakionya dhidi ya kuziamini Marekani na nchi za Magharibi. Mkakati wa Washington wa kuzidisha shinikizo dhidi ya Iran umechukua sura nyengine katika mfumo wa kisiasa nchini Iran na kutumiwa na wafuasi wa siasa kali kuwatia kishindo pia wafuasi wa siasa za wastani.

Zarif hakuarifiwa kuhusu ziara ya Bashar al Assad mjini Teheran

Wahafidhina wenye kufuata misimamo shupavu wakapata nguvu. Hilo limedhihirika jumatatu pale rais wa Syria Bashar al-Assad alipokaribishwa na kiongozi wa kidini wa Iran Ali Khamenei mjini Teheran. Lakini mkuu wa diplomasia ya Iran, Zarif hakuwa pamoja nao; baadhi wanasema; hata hakuarifiwa. Pamoja nao aliketi badala yake meja jenerali wa kikosi maalum cha walinzi wa mapinduzi Qassem Soleiman, kinachoendesha shughuli zale nchi za nje.

Kwa kujiuzulu Jawad Zarif makubaliano kuhusu mradi wa nuklea wa iran unampoteza pia mtetezi wake muhimu mjini Teheran.Tafiti 13 zilizosimamiwa na shirika la kimataifa la nishati ya nuklea IAEA zimebainisha Iran hadi wakati huu inaheshimu makubaliano hayo licha ya kujitoa Marekani. Hayo yamethibitishwa hivi karibuni pia na idara za upelelezi za Marekani. Mambo yanaweza kubadilika lakini. Pindi uamuzi wa kujiuzulu Zarif ukikubaliwa, basi ulimwengu hautakuwa tena mahala salama.

 

Mwandishi:von Hein,Matthias/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Sekione Kitojo