1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ushirikiano wa kimkakati ndiyo jawabu kwa ISIL

Iddi Ssessanga23 Juni 2014

Mafanikio ya kundi la wapiganaji la ISIL nchini Iraq yameitikisa mashariki ya kati. Mataifa ya magharibi yanapaswa kujitahidi kudhibiti machafuko yanayotokea kwa uyakinifu, anasema mwandishi wa DW Loay Mudhoon.

https://p.dw.com/p/1CO5T
Deutsche Welle Kultur Hintergrund Qantara Loay Mudhoon
Picha: DW

Bila shaka kuibuka kwa ghafla kwa kundi la ISIL kumebadilisha sura ya mambo katika kanda ya mashariki ya kati, kwa sababu wapiganaji hao wa jihadi walifanikiwa katika kipindi cha siku chache tu kuyadhibiti maeneo makubwa, na bila kukumbana na upinzani wowote wa maana kutoka jeshi la Iraq. Miongoni mwa maeneo hayo ni mji wa Mosul ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraq.

Wakati huo huo, wapiganaji hao wa ISIL wanaonekana kuimarisha udhibiti wao wa maeneo yanayokaliwa na wasunni magharibi mwa Iraq, na tayari wanadhibiti maeneo makubwa mashariki mwa Syria kwenye mto Euphrets. Zaidi ya hayo, wamefanikiwa kukiteka kivuko muhimu kwenye mpaka na Syria, hivyo katika hali halisi mpaka baina ya mataifa hayo mawili, ambamo kundi hilo linataka kuunda utawala wa Khalifa haupo tena.

Je, kushindwa kunakoendelea kwa mazaifa ya Iraq na hata Syria kunaashiria mwisho wa mgawanyo wa Sykes-Picot, kama wanavyoanza kubashiri baadhi ya waangalizi na wachambuzi wa masuala ya mashariki ya kati? Na kama ndiyo, nini kitafuata baada ya utaratibu huu uliyofuatia utawala wa Ottoman?

Kwa ukumbusho ni kwamba mfumo wa mataifa ya mashariki ya kati tunaoujua sasa, ulitokana na makubaliano yaliyosainiwa Januari 1916, kati ya Muingereza Mark Sykes na Mfaransa Francois Georges-Picot, ambayo ndiyo yaliunda jiografia ya kisiasa ya kanda hiyo hadi hii leo. Mataifa ya sasa yaliyoko kati ya bahari ya Mediterrani na mto Tigris yalitokana na makubaliano hayo na makubaliano mengine yaliyosainiwa baada vita vikuu vya kwanza vya dunia.

Udhaifu wa mataifa kama tatizo kuu

Ingeonekana kwamba kusonga mbele kwa kundi la ISIL nchini Iraq ni kitisho kikubwa cha kigaidi kwa kanda. Lakini ukilitafakari kwa kina, ni wazi kwamba tukio hilo ni ishara tu ya matatizo makubwa yaliyoikabili kanda ya Masahriki ya Kati.

Hali tete ya mataifa imeendelea kuwa tatizo kuu. Udhaifu wa mataifa ya kiarabu baada ya ukoloni ulibainika wazi miaka mitatu iliyopita, kufuatia mavuguvugu ya umma hususani nchini Libya na Syria.

Awali, utawala dhaifu wa George uliitumbukiza Iraq katika machafuko kupitia makosa yake ya mara kwa mara. Na juu ya hayo, hatua ya Marekani kumuunga mkono Nouri al-Maliki ilithibitika kuwa kosa kubwa. Waziri mkuu huyo wa Kishia anahusika binafsi kuitumbukiza nchi hiyo katika machafuko, kutokana na sera zake za kibaguzi dhidi ya Wasunni na Wakurdi - na hivyo kwa kuanguka kwa Iraq baada ya Saddam Hussein. Sera za Maliki za kuwatenga wengine ndiyo ziliweka mazinginra ya kuibuka kwa ISIL na makundi mengine ya wapiaganaji.

Ushirikiano wa kimkakati wahitajika

Migogoro hii inachochewa na mapambano ya kutaka ushawishi kati ya Iran na Saudi Arabia. Mgogoro huu wa ushawishi umeamsha hisia za uadui wa zamani kati ya Wasunni na Washia. Uhasama baina ya madhebu haya mawili umekuwa uktumiwa kama nyenzo ya kisiasa, na kuziba njia zote za utatuzi wa migogoro kwa busara.

Baada ya kushindwa nchini Syria, na ili kudhibiti migogoro ya kuvuka mipaka inayotokana na harakati za ISIL, ushirikiano wa kimkakati ndiyo jawabu kuu.

Kwa namna yoyote ile, viongozi mjini Tehran na Riadh wanaonekana kutambua ukweli kwamba kundi la ISIL lisilo na udhibiti kabisaa linaweza kuwa tishio kwa mataifa hayo mawili. Bila shaka hawahitaji kuona mataifa ya kanda yakianguka.

Kwa kuzingatia nafasi dhaifu yaliyomo kwa sasa, mataifa ya magharibi hayatarajiwi kurejesha utulivu kama nguvu ya nje, na badala yake yatategemea ushirikiano wa mataifa ya kanda. Marekani inapaswa kutmia njia za moja kwa moja za mawasiliano kati ya rais wa Iran Hassan Rouhan na mfalme Abdallah wa Saudi Arabia kuwezesha kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Iraq, bila kumhusisha Nuri al-Maliki alieshindwa.

Katika mazingira bora, hii inaweza kuwa hatua ya kwanza ya kusanifu upya ushirikiano katika kanda ya mashariki ya Kati. Taifa haliwezi kuundwa na wapiganaji wa jihadi - na ndiyo maana bado ni mapema mno kuzungumzia mwisho wa mfumo wa Sykes-Picot.