1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ulaya imechelewa kuingia Mali

18 Januari 2013

Hatimaye ushiriki wa Ulaya kwenye mgogoro wa Mali unaanza kuonekana kwa kutuma wakufunzi 250 kuwafunza wanajeshi wa Mali na kuwawezesha kupambana na wanamgambo wa Kiislamu nchini humo lakini umechelewa.

https://p.dw.com/p/17MjW

Imechukua kadhaa kwa Ulaya kufikia uamuzi huo, huku makundi ya Kiislamu yakiwa tayari yameshajijengea himaya yake kaskazini mwa Mali.

Kwa miezi yote hiyo, makundi hayo ya Kiislamu yametawala kwa kutumia tafsiri yake ya Sharia kwa kuvitia vijiji vya huko kwenye mateso ya kigaidi yakiwemo mauaji, ubakaji na wizi katika nchi iliyowahi kubeba bendera ya kuwa taifa la kidemokrasia magharibi ya Afrika.

Mhariri Mkuu wa DW, Ute Schaeffer.
Mhariri Mkuu wa DW, Ute Schaeffer.Picha: DW/P. Henriksen

Vurugu hizi, hapana shaka, zisingeliweza kushughulikiwa na umangimeza wa kutunga na kuangalia sera. Ndio maana Wafaransa walipoliona hilo, wakaamua kuchukua hatua peke yao, huku mataifa mengine ya Ulaya yakiendelea na utaratibu wa kulipigia kura na kujichimbia kwenye ubinafsi wao.

Umma wa Ufaransa wanaliunga mkono hili, na ambalo sasa linaungwa mkono pia na Umoja wa Mataifa, bila ya kinyongo chochote.

Lakini Ujerumani je?

Kuna uchaguzi mkuu unaokuja, na sera za wapigania uchaguzi huo zinataka kulikwepa hili kadiri iwezekanavyo. Lakini umma wa wapiga kura wa Ujerumani, kutokana na midahalo inayopamba moto kwenye vyombo vya habari, unalijua hilo. Ndio maana, maana ya kujikongoja siku nyingi, hatimaye nayo Ujerumani inatuma ndege zake mbili tu za mizigo.

Lakini hilo halitoshi. Uamuzi madhubuti zaidi lazima uchukuliwe na bunge. Na yumkini kelele zetu kwenye vyombo vya habari zitasadia kufikiwa kwa uamuzi huo, ikiwa tutasimama imara kama waandishi na raia wa nchi hii, kwa kufahamu kwamba Mali sio nchi iliyo kwenye jangwa tu magharibi mwa Afrika.

Karibu nusu karne baada ya Ujerumani mbili kuungana tena, katika wakati dunia ikikabiliwa na migogoro kadhaa, lazima Ujerumani iwe na sera yake maalum ya usalama kuelekea bara la Afrika, maana hili ni bara lililo jirani yetu kabisa. Ni aibu kwamba hatuna taarifa za kutosha kulihusu.

Mali si nchi ya jangwani tu

Katika vyombo vya habari vya Ujerumani, picha pekee ya Mali ni mabaki ya dola la Sahel. Lakini ukweli ni kuwa nchi hiyo ina uwezekano wa kuwa bomu la eneo hilo. Ikiwa Mali itaharibikiwa, eneo zima la Sahel, ambalo linaiunganisha magharibi na kaskazini ya Afrika itaripuka moto.

Na eneo hilo haliko mbali sana na Ujerumani, kama wengine wanavyotaka kudhani. Ikiwa moja ya mataifa yenye eneo kubwa, Mali inapaswa kupigana kulinda mipaka yake saba, ambako nyingi ya nchi inazopakana nazo tayari zina matatizo kadhaa: tangu umasikini hadi ukosefu wa taasisi imara za kiutawala na hivyo kuyafanya makundi ya kigaidi na uhalifu kuimarika.

Hata hivyo, kuna nukta mbili za kuzizingatia hapa: Moja ni kwamba operesheni ya kijeshi nchini Mali ina hatari zake nyingi na kubwa, hasa kwa wanajeshi wa ardhini wa Ufaransa wale 3,300 wa Afrika ya Magharibi waliotumwa huko.

Lakini pili ni kuwa ukubwa wa hatari hiyo hauwezi kulinganishwa na hatari kubwa zaidi inayoweza kutokea huko mbeleni, ikiwa hatua hizi hazikuchukuliwa sasa.

Tukio la kuchukuliwa mateka kwa wafanyakazi wa kigeni na wenyeji wa kampuni ya gesi kusini mwa Algeria ni mfano halisi unaohalalisha hatua ya kijeshi ya Ufaransa nchini Mali.

Mwandishi: Ute Schaeffer/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo