1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani imebadilika

5 Septemba 2016

Bado wananchi wengi wanaiunga mkono kauli ya Kansela wao Angela Merkel ya "tutaweza" lakini lawama juu ya sera yake ya wakimbizi zinaongezeka anasema mwandishi wetu Verica Spasovska katika maoni yake

https://p.dw.com/p/1JuqF
Wakimbizi nchini Ujerumani
Wakimbizi nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/S. Kahnert

Yapo mambo yaliyobadilika nchini Ujerumani mnamo mwaka huu.Kwanza kabisa habari mbaya:ubaguzi umeongezeka nchini.

Chama cha mrengo wa kulia cha AfD kilichoanza kupungukiwa wafuasi kabla ya mgogoro wa wakimbizi ,sasa kinajinufaisha kutokana na hofu za Wajerumani wengi juu ya wakimbizi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni chama hicho sasa kinaungwa mkono kwa asilimia 15 nchini Ujerumani kote.

Katika uchaguzi wa bunge uliopita chama hicho hakikuweza kukiruka kiunzi cha asilimia tano na hivyo kushindwa kuingia katika Bunge kuu la Ujerumani.Lakini sasa mambo yamegeuka. Chuki dhidi ya wahamiaji umekuwa mtindo nchini Ujerumani.

Ujerumani ni tofauti kulinganisha na nchi nyingine

Hata hivyo mtu anapaswa kuulinganisha ukweli huo katika muktadha wa Ulaya nzima: nchini Ufaransa na Bulgaria vyama vya mrengo wa kulia vinawakilishwa kwa asilimia 20 kwenye mabunge ya nchi hizo na nchini Poland na Hungary wawakilishi wa kambi za mrengo wa kulia wamo serikalini.

Mwandishi wa maoni Verica Spasovska
Mwandishi wa maoni Verica Spasovska

Nchi Uingereza chama kinachowapinga wahamiaji cha UKIP ndicho kilichoichochea kampeni juu ya nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya.Kulinganisha na nchi za Ulaya Mashariki ambako itikadi za kizalendo zimeota mizizi, Ujerumani ni nchi yenye siasa za wastani na pia ni nchi ya utulivu.

Hata hivyo uhusiano baina ya wananchi na Kansela wao umebadilika. Umaarufu wake umeshuka.Wajerumani wengi hawaridhishwi na jinsi mgogoro wa wakimbizi unavyoshughulikiwa.Lakini umaarufu wa vyama ndugu vilivyomo katika serikali bado ni imara. Kansela Angela Merkel bado anapewa hadhi ya juu katika siasa za mambo ya nje.

Hata ikiwa, sera yake ya wakimbizi, haiungwi mkono katika nchi nyingi za Umoja wa Ulaya, neno lake bado lina uzito katika masuala muhimu, kama vile juu ya kuamua namna ya kusonga mbele baada ya Uingereza kuamua kujiondoa Umoja wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel amepongezwa kwa ubinadamu wake kwa kuwapokea wakimbizi siyo na Rais Obama tu. Ujerumani imesimama katika upande sahihi wa historia.Inapongezwa pia na watu wengi barani Afrika na katika nchi za Mashariki ya Kati.Sababu ni kwamba Ujerumani ilizitekeleza kauli kwa matendo kwa kuwakaribisha watu waliokuwamo katika dhiki.

Hata hivyo mambo yamebadilika. Baada ya moyo mkubwa wa kuwa tarayi kusaidia hapo mwanzoni, sasa watu wamezibuka macho katika sehemu nyingi za jamii.

Matukio ya mkesha wa Krismasi ambapo wanawake walibughudhiwa, na mashambulio yaliyofanywa na magaidi wenye itikadi kali ya kiislamu katika miji ya Ansbach na Würzburg yamesababisha hofu miongoni mwa Wajerumani hata ikiwa waliofanya mashambulio hayo tayari walikuwapo nchini Ujerumani kabla ya kuwasili kwa wakimbizi mwaka uliopita.

Leo tunajua kwa uhakika kwamba Waislamu wenye itikadi kali pia waliitumia fursa ya ukarimu walioonyeshwa wakimbizi na kujipenyeza nchini mwaka uliopita.Lakini laiti mipaka ingefungwa maalfu ya watu waliokuwa wanahitaji msaada wasingelisaidiwa. Licha ya hali ya wasi wasi moyo wa kuwasaidia wakimbizi bado ni mkubwa nchini.

Wajerumani wanasaidia kwa kadri inavyowezekana. Kwa mfano wanasaidia katika kuwafundisha wakimbizi lugha ya kijerumani.Au wanawasaidia katika juhudi za kutafuta ajira. Moyo huo mkubwa wa ukarimu katika kuwakaribisha wakimbizi waliokuwamo katika hali ya dhiki,unaweza kuzingatiwa na Ujerumani kwa haki kabisa kuwa ni mafanikio.

Lakini changamoto bado zipo .Watoto wa wakimbizi wanahitaji kwenda shule na wazazi wao wanahitaji kutangamanishwa na jamii ili waweze kupata ajira.Hizo zote ni gharama zinazoweza kusababisha roho ya kijicho na hivyo kuvuruga amani ya jamii.

Ikiwa Wajerumani hawatawazingatia wakimbizi kuwa tatizo, na badala yake kuyaangalia mambo kwa uhalisia wake, na ikiwa watatambua kwamba kushikamana na watu wenye dhiki,kunaweza kuimarisha umoja, tutaweza kupima na kusema, kweli, ni jambo zuri kwamba Ujerumani imebadilika!

Mwandishi: Spasovska,Verica

Mfasiri: Mtullya Abdu.

Mhariri: Sudi Mnette