1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Trump anaweza kushinda vita hii

28 Agosti 2020

Baada ya Trump kukubali uteuzi wa chama cha Republican kugombea urais kampeni zinaweza kuanza kwa uongo, hofu na ghasia. Hii inaweza kusababisha Trump achaguliwe tena, anaandika Ines Pohl mwandishi wa DW, Washington.

https://p.dw.com/p/3hdDW
USA Nominierungsparteitag der Republikaner | Donald Trump
Picha: Reuters/C. Barria

Ni kawaida katika demokrasia ya vyama kuwachagua wagombea wao wa juu katika mkutano mkuu wa chama. Lakini matukio makubwa nchini Marekani, ambako vyama vya Republican na Democratic vinaadhimisha kwa siku kadhaa, ni jambo la kawaida kabisa kwa Wamarekani. Hata kama washindi wa nafasi za awali wameshajulikana kwa miezi kadhaa, wagombea husika wamekubali uteuzi wao kwa ishara nzuri na maneno mengi.

Washindani hutumia majukwaa kuwasilisha sera zao za kisiasa na kuwaelekeza wapiga kura walioshawishika na wasio na msimamo katika sanduku la kura. Wakati rais aliyeko madarakani tayari kamaliza awamu ya kwanza kati ya mbili anazoruhusiwa kisheria kuwa nazo, anatumia jukwaa na madaraka aliyonayo kuonyesha yale ambayo tayari ameyafanikisha na kile ambacho bado anataka kukitimiza.

Kwa kawaida, hili huambatana na kupongezwa, mapumziko na shamrashamra. Lakini mwaka huu wakati wa janga la virusi vya corona, kila kitu ni tofauti. Mikusanyiko mikubwa haifanyiki kwenye nchi hiyo yenye idadi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo. Timu zote za kampeni zimelazimika kuzindua kampeni za kuingia Ikulu ya Marekani katika wakati mgumu wa mapambano.

USA Präsidentschaftskandidat Joe Biden in Wilmington, Delaware
Joe Biden, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha DemocraticPicha: Reuters/K. Lamarque

Aliyeshindwa tayari anajulikana: Watu wa Marekani

Bado haiwezekani kusema ni nani aliyezijua vyema changamoto hizi ambazo hazikuwepo zamani. Vyama vyote vya Republican na Democratic vinataka mgombea wao ashinde, kwani vimekuwa vikiwavutia wapiga kura wote, hata wale ambao bado hawajaamua.

Hata kama matukio haya hayamuonyeshi mshindi, aliyeshindwa tayari anajulikana: Watu wa Marekani ambao wanaishi kwenye jamii ambayo hata haiwezi kukubaliana kuhusu sheria za msingi za kuishi pamoja.

Rais Donald Trump anapuuza maoni au hisia za watu wengine. Mtu yeyote ambaye anamuuliza kuhusu uongo au upotoshaji wake, iwe ni mwandishi habari au mwanasayansi, anadharauliwa kama mtu anayeeneza chuki au mdhalilishaji.

Kuna idadi kubwa ya Wamarekani ambao wanaamini tu kile kinachowafaa kwenye ulimwengu wao. Takwimu mbaya za kiuchumi zinatengenezwa ziwe za kuvutia, wanaharakati wa njama wanazibadilisha nchi nyingine kuwa mataifa hatari ambayo yanataka kuitawala Marekani, huku virusi hatari vinavyosababisha vifo vikiwa havizungumziwi ipasavyo.

Maonyesho badala ya ukweli

Mikutano ya chama imeangazia zaidi jinsi Marekani ilivyogawanyika na namna siasa za uongo za utawala wa Trump zimeendeshwa katika miaka michache iliyopita. Sasa kipindi cha kampeni kinaanza. Mapambano kama ambayo hayajawahi kutokea hapo kabla.

Ines Pohl
Ines Pohl, mwandishi wa DW mjini WashingtonPicha: DW/P. Böll

Wiki chache zijazo, tutashuhudia jinsi demokrasia inavyojieleza Marekani kuhusu uwezo wa kuchukua madaraka. Baada ya mikutano hii ya vyama mtu anapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu nini maana ya demokrasia iwapo mtu anayefuata siasa kali za kizalendo, atachaguliwa tena? Je huu utakuwa mtindo wa dunia?

Tunaishi katika nyakati ambazo sio rahisi kwa jamii kukubaliana kuhusu ukweli wenye uzoefu kwa pande zote. Marekani inazidi kuwa kama kipindi halisi cha televisheni, inajaribu kuwapa washiriki wake, raia wake, hisia kwamba wao ni mashujaa. Hata kama hilo halihusiani na ukweli.