Maoni: Trump ameiruhusu Saudi Arabia kutoadhibiwa kwa mauaji
21 Novemba 2018Matamshi na mitizamo ya kiholela kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi yanayotolewa na Ikulu ya Rais wa Marekani ya White House ni bayana kuwa vinatoka kwa Rais Trump mwenyewe, na ujumbe anaoutoa ni kuwa huenda Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohamed Bin Salman ndiye aliyeagiza mauaji hayo katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, lakini sijali na sitaruhusu mauaji yaliyopangwa ya mwandishi huyo kuhujumu manufaa ya kibishara na kiuchumi ya Marekani kutoka kwa Saudi Arabia na kuiandama Iran.
Ingekuwa ni kiongozi mwingine mbali na Trump angeulizwa maswali mawili. Je huna mhariri na je, nafsi yako haikusuti? Kwa Trump maswali haya hata hayamjalishi, anaonekana kutokuwa na utashi wala urari wa kufuatilia hoja za kimsingi na wala hajali hata chembe kuhusu lililo jema wala baya.
Nafsi haimhukumu?
Lakini kutokuwa na uelewa au kutotaka kufuatilia yanayostahili au yote mawili yaani kutofautisha kuhusu baya na lililo jema hakumpi kisingizio, hasa kiongozi wa dola lenye nguvu zaidi duniani.
Hii si hulka wala matarajio ya kiongozi wa Marekani, taifa ambalo kwa miaka mingi limekuwa ikijivunia kuwa na viongozi wanaotambua wapi pa kuchora mpaka kati ya jema na baya hata kama saa nyingine hawakutekeleza kikamilifu walichojivunia.
Trump ni tofauti, hata hajifanyi kuwa kiongozi mwenye maadili, kama alivyodhihirisha kuwa biashara na Saudi Arabia na vita vyake dhidi ya Iran vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia ni muhimu sana kwake kuliko kuchukua hatua ili haki itendeke kutokana na mauaji ya kinyama ya Khashoggi mwandishi wa gazeti la Marekani la Washington Post, gazeti ambalo Trump analidharau.
Tabia hii ya Trump haishangazi lakini ni uthibitisho mwingine juu ya aina ya mtu waliemchagua Wamarekani miaka miwili iliyopita.
Trump kupuuzilia mbali ushahidi wote na ripoti za kijasusi kuwa viongozi wa Saudi Arabia walihusika katika mauaji ya kinyama ya Khashoggi na kukataa kuichukulia nchi hiyo hatua kali zinazostahili, anaendekeza maovu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia.
Na sio tu kuipa Saudi Arabia nguvu ya kuendelea na ukiukaji huo, bali pia anawapa nguvu madikteta wengine duniani kudharua sheria, na kufanya vitendo kama vya Saudi Arabia. Trump ameifanya tarehe 20 Novemba 2018, kuwa siku ya simanzi kubwa duniani kwa kudharau haki za binadamu, na hili halipaswi kuvumiliwa hata kidogo!
Mwandishi: Michael Knigge/ https://p.dw.com/p/38d5t
Tafsiri/Msimulizi: Caro Robi
Mhariri: Iddi Ssessanga