1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rouhani, Ahmedinejad wa pili?

24 Julai 2018

Kwa kujibizana uchokozi na Rais wa Marekani Donald Trump, Rouhani haonyeshi mkururo wowote wa ahadi alizozitoa kwa Wairan mwaka 2013. Badala yake, anaonekana kuwa mwenye misimamo mikali zaidi, anasema Jamshid Barzegar.

https://p.dw.com/p/320Kt
Iranischer Präsident Hassan Rouhani
Picha: Reuters/L. Niesner

Matamshi ya karibuni ya Rais Hassan Rouhani wa Iran kuhusu uwezekano wa kufunga njia ya bahari ya Hormuz inayotumiwa kwa usafirishaji wa mafuta yanakwenda kiunyume kabisa na ahadi alizozitoa kwa raia wa Iran mwaka 2013. Badala yake yanafanana na yale yaliokuwa yakitolewa na mtangulizi wake, Mahmoud Ahmadnejad.

Katika mazingira ya nyumbani, Rais Rouhani amekuwa akitekeleza ahadi zake za kampeni kwa kiasi kikubwa. Lakini katika ngazi ya kimataifa, nini kinamfanya achaguwe matamshi makali yaliyotumiwa Ahmadnejad, licha ya ukosoaji wa mara kwa mara wa mtindo wa kiongozi huyo wa zamani na kutaja kipaumbele chake kuwa ni kutatua migogoro ya Iran na mataifa ya magharibi kupitia majadiliano?

Kuzungumza na hadhira ndogo

Yaonekana mambo tofauti yamepelekea kubadilika kwa msimamo wa Rouhani kuhusu sera ya kigeni, ambayo yote yamemfanya achaguwe kumridhisha kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na makamanda wa kikosi cha ulinzi wa Jamhuri kuliko watu waliomchagua.

Kwanza kabisa, maandamano makubwa yaliosambaa katika maeneo mbalimbali ya Iran yanaweza kuhusishwa na kubadilika kwa sera yake. Maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika kupinga uhaba wa maji na umeme, mgogoro wa sarafu, ukosefu wa ajira na rushwa iliokithiri miongoni mwa maafisa wa serikali ya Iran.

Pili, kujiondoa kwa Marekani katika mkataba wa nyuklia na Iran na mabadiliko katika baraza la mawaziri la Trump vimesababisha wasiwasi mjini Washington, na kuepelekea kuchukuliwa msimamo mkali zaidi dhidi ya Iran.

Zaidi ya hapo, uhasama wa karibuni wa Marekani dhidi ya Iran umekwenda mbali kiasi kwamba Trump na waziri wake wa mambo ya ndani Mike Pompeo wamedai waziwazi kusaidia kuandaa maandamano makubwa nchini Iran, na kuapa kuwaunga mkono waandamanaji.

Jamshid Barzegar -  neuer Leiter der DW Farsi-Redaktion.
Jamshid Barzegar ni mkuu wa idhaa ya Kifarsi ya DW.Picha: DW/B. Scheid

Aidha, kitisho cha utawala wa Trump kuzuwia mauzo ya nje ya mafuta ya Iran kuanzia Novemba 2018 - kikiambatana na juhudi za kuweka kile ambacho Trump amekitaja kuwa vikwazo vya kihistoria dhidi ya Iran pamoja na shinikizo linalozidi kwa washirika wa Iran kupunguza biashara na taifa hilo -- vinakumbushia miaka ya mwisho ya urais wa Ahmadnejad.

Sifa kutoka ngazi za juu

Kinachosalia kuwa sawa na misimamo iliochukuliwa na Ali Khamenei, ambaye kwa kawaida anakataa kumuunga mkono wazi Rouhani, lakini hivi karibuni amemsifu rais huyo kuhusiana na matamshi yake juu ya kuifunga njia ya Hormuz. Kiongozi huyo mkuu alimtaka hata waziri wa mambo ya nje kuchukuwa msimamo sawa; na mkuu wa kikosi maalumu cha Quds, Qasem Soleimani, pia alisifu tamko la Rouhani kuhusu Hormuz katika barua.

Inaonekana kwa upande mmoja, kwamba nafasi ya wanasiasa wa msimamo wa wastani na wanamageuzi imepungua pakubwa miongoni mwa wapigakura katika miezi ya karibuni. Kwa upande wa pili, badala ya kujaribu kuiimarisha, Rouhani anataka kuimarisha nafasi yake ndani ya mfumo wa madaraka.

Biashara hatari

Na njia ipi bora zaidi ya kuimarisha nafasi yake ndani ya mfumo wa madaraka kuliko kuboresha uhusiano wake na wanasiasa wa msimamo mkali? Ili kufanya hivyo, Rais Rouhani siyo tu amerejelea sera za Ahmadnejad, lakini pia amekwenda mbali zaidi kwa kurudia matamshi ambayo yalitolewa tu na Saddam Hussein: "Mgogogoro wowote na Iran, ndiyo mama wa vita vyote." Kiongozi huyo wa zamani wa Iraq alianzisha uchokozi muda mfupi tu kabla ya uvamizi wa Marekani mwaka 2013 -- na historia imeonyesha namna ilivyokwenda.

Wakati mkakati mpya wa Rouhani unaonekana kujikita katika kuwafurahisha wanasiasa wenye msimamo mkali nyumbani, madhara yake hayatabakia tu nyumbani, kama majibu makali ya Trump yalivyoonesha. Kwa uchache zaidi, yataongeza mashaka miongoni mwa washirika wa Ulaya wanaohangaika kuunusuru mktaba wa nyuklia wa Iran -- na kupanda mbegu zaidi za uadui katika mazingira ya kimataifa ambayo tayari yamejaa wasiwasi.

Mwandishi: Jamshid Barzigar

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Mohammed Khelef