1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Pale ushindi usipomaanisha ukombozi

7 Mei 2020

Majanga, teknolojia, uhamiaji na mabadiliko ya tabia nchi, ndivyo vitatengeneza mawazo ya kisiasa ya karne ya 21, kuliko kumbukumbu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

https://p.dw.com/p/3buQd
Monument Polen Zweiter Weltkrieg Gefallene
Picha: Imago Images

Kumbukumbu za Vita Kuu ya Pili ya Dunia zinafifia wakati kizazi ambacho kilishuhudia vita kinatoweka. Mei mwaka uliopita utafiti wa maoni uliofanywa na Baraza la Ulaya la Uhusiano wa Kigeni kwenye nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya, uligundua kwamba watu wa Ulaya wenye umri kati ya 18 hadi 24 wana uwezekano mkubwa wa kuamini kuwa vita kati ya nchi za Ulaya vinaweza kutokea tena miaka 10 hadi 20 ijayo.

Msimamo huu unaashiria kumalizika kwa ulimwengu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia hata kabla ya virusi vya corona havijaripuka. Mshairi wa Kimarekani, Charles Simic anaandika, pengine sababu ya kutojifunza kutokana na historia, hatukubaliani na ukweli kuhusu vita na madhara yake, kwa hofu kwamba ikiwa tutafanya hivyo, tutaacha kumwamini Mungu na binadamu wenzetu.

Miaka 75 baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, hakutakuwa na maadhimisho makubwa kwenye mji wowote mkuu wa Ulaya kwa sababu ya janga la COVID-19. Lakini sio virusi vya corona tu, pia ni virusi vya marekebisho ya kihistoria ambavyo vimelikumba bara la Ulaya. Tunachoshuhudia nchini Urusi na baadhi ya nchi za Ulaya Mashariki ni kumbukumbu za silaha za vita. Kukataa simulizi za serikali inachukuliwa kuwa ni uhalifu.

Vita juu ya ukweli na kumbukumbu

GMF Speaker Ivan Krastev
Ivan Krastev anasema muhimu sio ushindi, lakini ukomboziPicha: IWM/Klaus Ranger & Zsolt Marton

Vita vya propaganda kuhusu Vita Kuu ya Pili ya Dunia haviifanyi Urusi, wala baadhi ya serikali za Ulaya Mashariki kuonekana nzuri. Katika Ikulu ya Urusi, simulizi yoyote inayopinga ukaliaji wa mabavu wa Kisovieti Ulaya Mashariki baada ya mwaka 1945, ni fashisti na ukosoaji wowote wa sera za Stalin ni jaribio la makusudi la kudhoofisha jukumu muhimu la jeshi la Kisovieti la Red Army katika kumshinda Adolf Hitler.

Kuna simulizi nyingi kuhusu Ulaya Mashariki ambazo zinaiwakilisha ile ya Urusi - kwamba kila mtu aliyepigana dhidi ya Wasovieti, wakiwemo waliokuwa washirika wa utawala wa Kinazi, wanasifiwa kama mashujaa.

Lakini historia ni ngumu zaidi. Kama Mkurugenzi Mkuu wa wakfu wa Buchenwald, Volkhard Knigge alivyomwambia mwanafilosofia wa Kimarekani, Susan Neiman aliyeandika kitabu cha "Kujifunza kutoka kwa Wajerumani", ili simulizi hii nyeupe na nyeusi iwe ya kweli, "inabidi uwe na kambi za mateso bila Wakomunisti na kambi ya Kisovieti bila Manazi." Lakini Buchenwald, ambayo ilikuwa kambi ya mateso wakati wa utawala wa Manazi na kambi ya Kisovieti baada ya vita, ni mfano mzuri kwamba kambi sahihi za kisiasa sio tu simulizi za uongo.

Maana ya ukombozi

Kwa kawaida vita hutokea katika maeneo. Kumbukumbu za vita kati ya Urusi na Ukraine, Urusi na Poland au Urusi na Jamhuri ya Czech, ni zaidi ya maana ya neno "ukombozi. " Mwaka 1985, Rais wa Ujerumani Richard von Weizsäcker aliweka historia kwa kuitangaza Mei 8 kuwa Siku ya Ukombozi wa Ujerumani.

Aliwaambia washirika wake kwamba wakati ni kweli Wajerumani pia wameteseka sana wakati wa vita na haki haijatendeka kwa Wajerumani baada ya vita, Wajerumani hawana haki ya kujiita wenyewe wahanga, kwa sababu wanahusika na mateso makubwa ya wengine na kwa sababu ya mauaji ya Wayahudi.

Ni somo hili la Ujerumani ambalo limepotea kwenye Ikulu ya Urusi leo. Kinachoifanya Ulaya Mashariki na Kati kuwa tofauti na Ulaya Magharibi linapokuja suala la kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia ni kwamba Ulaya Mashariki haiwezi kuitangaza Mei 8, mwaka 1945 kuwa siku ya ukombozi wao.

Kuwasili kwa jeshi la Kisovieti ilikuwa ni ushindi dhidi ya utawala wa Kinazi nchini Ujerumani, lakini haikuzikomboa nchi zao. Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekataa kukubali ukweli kwamba mamilioni ya watu wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti walikufa wakati wakiwaendesha Wanazi kutoka Ulaya Mashariki, hali hii haiipi Urusi haki ya kuamua lini nchi za Ulaya Mashariki zinapaswa kusherehekea ukombozi wao.

Deutschland Gedenken 75. Jahrestag der Buchenwald-Befreiung
​​​​Kambi ya BuchenwaldPicha: picture-alliance/dpa/M. Gentzel

Haikuwa washirika, lakini rais wa Ujerumani ambaye miaka 40 baada ya kumalizika kwa vita, aliitangaza Mei 8 kuwa Siku ya Ukombozi. Na ni wananchi wa Ulaya Mashariki ndiyo wataamua nini cha kuita siku yao ya ukombozi.

Ivan Krastev ni mwanasayansi wa siasa wa Bulgaria. Ni mwenyekiti wa Kituo cha Mikakati cha ukombozi mjini Sofia na mshirika wa kudumu katika Taasisi ya Sayansi ya Binadamu mjini Vienna. Kitabu chake cha hivi karibuni alichokiandika kwa kushirikiana na Stephen Holmes kinaitwa, "Nuru Iliyoshindwa. "

(DW https://bit.ly/3bcvL1B)