Maoni : Ni Clinton ama Trump uchaguzi Marekani
7 Novemba 2016Dunia inasubiri kwa hali ya wasi wasi , wakati Marekani itakapochagua rais wake mpya. Na bado inawezekana kwamba Trump huenda akahamia katika Ikulu ya White House na mkewe Melania na jamaa wengine wa familia yake tajiri. Uwezekano huo binafsi ni hali inayoleta wasi wasi. Kwa nini linatokea hili ? Wamarekani wana matatizo gani ? Inawezekanaje wakafikiria kuchagua mtu ambaye hana kabisa uzoefu wa kisiasa katika kiti chenye madaraka makubwa kabisa ya kisiasa duniani ?
Obama anaacha mlima wa mambo ambayo hayajatatuliwa. Majukumu ambayo hayajatatuliwa ambayo rais Barack Obama atakuwa anayaacha kwa mrithi wake ni makubwa, upande wa ndani ya nchi na upande wa masuala ya kigeni.
Mageuzi yake ya masuala ya afya bado hayajakamilika. Syria ni mfano mmojawapo wa ombwe la madaraka ambalo linatokea wakati polisi wa dunia Marekani wanajiondoa na hakuna mtu , isipokuwa Urusi , iko tayari kuingilia kati na kujaza ombwe hilo.
Hususan wakati Marekani ikishindwa kupata msaada wa kijeshi wa mataifa ya Ulaya ambapo Obama amejenga mkakati wake mpya wa kujizuwia.
Hatimaye inawezekana kwamba Hillary Clinton anaweza kushinda uchaguzi.
Uongozi wake katika maoni ya wapiga kura unayeyuka , lakini kwa bahati nzuri kuna hali hii ya aina ya kipekee ya mfumo wa uchaguzi wa Marekani , unaotegemea uhakika wa fungu maalum la kura katika kila jimbo kutokana na wingi wa wapiga kura wake, maarufu kama Electoral College.
Lakini mbali ya matokeo , tayari inaonekana wazi kwamba kutakuwa na walioshindwa tu wakati kinyang'anyiro hiki kitakapomalizika.
Katika miezi kadhaa iliyopita Marekani imegeuka kuwa nchi iliyojengeka katika dhana ya kula njama na fitina. Hilo linamhusu zaidi Donald Trump. Ni mtu ambaye hana wazo kabisa kuhusiana na masuala ya siasa za kibiashara. Lakini ana uwezo wa kuzungumza na kubadilisha shaka kuwa chuki, hofu ya kupoteza kuwa chuki dhidi ya wageni na kutokuwa na usalama kuwa hisia za kuwa na madaraka makubwa. na ana uwezo wa kujinasibisha kuwa ni mkombozi pekee wa nchi hiyo. Hii ni njia ya ushindi ya fitina.
Kwa sababu hiyo watu wengi duniani wanaelekeza kukatishwa kwao tamaa na wasi wasi juu ya hali nchini Marekani kwa Donald Trump. Wanamuona kama mtu anayehusika na kuiweka Marekani katika njia ya kutoweza kutawalika.
Lakini hilo si sahihi , takriban katika dhana ya kisiasa. Trump sie mwanasiasa , ambaye kwa tafsiri anataka kuimarisha mambo lakini anayeweza kumaumika iwapo atashindwa kufanya hivyo. Trump ni mfanyabiashara. Kwa hiyo lengo lake kuu ni juu ya vipi anaweza kubadili mambo kwa faida yake. Hivi ndivyo alivyoweza kuongoza biashara yake ya kuuza na kununua majumba, na hivi ndivyo alivyoshinda uteuzi wa chama cha Republican. Na , mtazamo huu huenda ukamfikisha Ikulu ya White House.
Mwandishi: Ines Pohl / zr / Sekione Kitojo
Mhariri : Yusuf Saumu