1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mkutano maalum wa chama cha SPD na kuchaguliwa Nahles

23 Aprili 2018

Mwenyekiti mpya wa chama cha Social Democratic (SPD) Andrea Nahles aliyechaguliwa hapo jana atakabiliwa na kazi ngumu. Matokeo ya uchaguzi yamebainisha ni kwa kiasi gani imani imepungua miongoni mwa wanachama wa SPD:

https://p.dw.com/p/2wUHE
Außerordentlicher Bundesparteitag der SPD
Picha: picture-alliance/dpa/B. Roessler

Matokeo ya kura yangelipaswa kuwa mazuri zaidi kwa mwanamke wa kwanza aliyechaguliwa kukiongoza chama cha Social Democratic katika historia ya miaka 155 ya chama hicho. Ni robo tatu tu ya wajumbe waliompigia kura mwanasiasa huyo mwanamke. Mwenyekiti aliyewahi kupata kura chache zaidi, alikuwa Oskar Lafontaine mnamo mwaka 1995. Ni jambo la kusikitisha kwa kweli.

Mwenyekiti mpya wa chama cha SPD Andera Nahles
Mwenyekiti mpya wa chama cha SPD Andera NahlesPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha SPD alipaswa kurindima. Hata hivyo matokeo hayo hayakusababishwa na kuwa yeye ni mwanamke, na wala wajumbe waliomyima kura zao hawakumlenga yeye binafsi bali matokeo hayo yanabainisha mpasuko mkubwa ndani ya chama cha SPD.

Wanachama wa chama hicho wamegawika juu ya njia ambayo chama chao inapaswa kupita ili kujijenga upya. Kuna kambi ya wale wanaoamini kwamba kuelekea kwenye mrengo wa kushoto zaidi ndio kutaweza kukikomboa chama chao. Yaani kurejea katika zama za chama cha tabaka la wafanyakazi na watu wa kawaida. Wajibu mkubwa zaidi wa serikali na ustawi wa jamii kwa wote na pia msingi wa usalama kwa wasio na ajira!

Mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles akizungumza na wajumbe wa chama chake
Mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles akizungumza na wajumbe wa chama chake.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kambi nyingine ni ya wanachama wanaotaka ujenzi mpya wa chama chao lakini siyo kwa kupitia njia ya mrengo mkali wa kushoto, yaani msimamo usiopinga kwa uwazi serikali ya mseto na vyama vya Christian Demokratic Union,CDU na Christian Social Union CSU.  Mwenyekiti mpya Andrea Nahles mwenyewe anaunga mkono njia hiyo.

Anataka chama cha SPD kiwe mshirika wa kuaminika katika serikal lakini wakati huo huo kiwe na muhuri wake wa kisiasa. Kuongoza na kujijenga upya. Uangalizi mkubwa unahitajika. Hata hivyo wachambuzi wanasema njia hiyo inaweza ikashindikana. Wachambuzi hao hawaamini iwapo Andrea Nahles kweli ataweza kukijenga upya chama cha SPD. Ni kweli kwamba yeye amekuwa mwanachama wa SPD kwa muda wa miaka 30 sasa. Ameshatumikia nyadhifa mbalimbali za chama chake na pia aliwahi kuwa waziri katika serikali iliyopita.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Katikati: Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer. Kulia: Mwenyekiti mpya wa SPD Andrea Nahles
Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Katikati: Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer. Kulia: Mwenyekiti mpya wa SPD Andrea NahlesPicha: picture-alliance/AP/M. Sohn

Nahles ni mwanasiasa anayetokea katika tabaka la watawala na hilo hasa ndilo tatizo linalomkabili. Ana vumba la yote yaliyokwenda mrama mnamo miaka iliyopita Jee itawezekana kwa mwanasiasa kama huyo kujijenga upya?

Thuluthi moja ya wajumbe hawakumpigia kura. Anatambua hayo na hilo si jambo la kushangaza. Isingelikuwa busara kwake kutumai kupata kura nyingi zaidi. Aliweza kuona kwenye mkutano mkuu wa chama chake uliofanyika mjini Bonn hivi karibuni, hoja ya kuunga mkono kujiunga na serikali ya mseto ilipita kwa chupuchupu tu.

Waliopinga hoja hiyo walikuwa na makusudi ya kutoa ishara kwa viongozi wa chama. Kutokana na hali hiyo matokeo ya uchaguzi wa jana yalikuwa ya dhati kwa Andrea Nahles kwamba umaarufu wa chama cha SPD umeanguka miongoni mwa wapiga kura. Andrea Nahles anapaswa kukikarabati chama chake na kuleta umoja. Hicho ndicho kitakuwa kipimo cha mafanikio yake.  

Mwandishi: Zainab Aziz/ Kinkartz, Sabine/ LINK: http://www.dw.com/a-43489502

Mhariri: Gakuba, Daniel