1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Merkel ataufuata mpango wa Macron?

19 Aprili 2018

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wanakutana kujaribu kutafuta mwelekeo katika suala la mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya, suala nyeti linaloipa mtihani serikali ya Ujerumani iliyoingia madarakani mwezi mmoja tu uliopita.

https://p.dw.com/p/2wJ5X
Frankreich Treffen Angela Merkel & Emmanuel Macron in Paris
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron tayari ameshaweka wazi mipango yake kuhusiana na Ulaya wakati alipozungumza katika bunge la Strasbourg hapo Jumanne. Alhamis anakutana na Kansela Angela Merkel mjini Berlin, mahala ambako mapendekezo yake tayari yamezusha mjadala mkali.

Kawaida haijawa hivi. Muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa Macron nia yake ya kuifanyia mageuzi Ulaya ilipokelewa vizuri sana nchini Ujerumani. Lakini miezi michache baadae baada ya uchaguzi wa Ujerumani, kuliibuka chama cha siasa za mrengo wa kulia cha AfD na kuingia bungeni. Chama hicho kilianzishwa kwa misingi ya kuipinga Ulaya. Baada ya hapo ukaja ule mkwamo wa kisiasa uliopelekea Ujerumani kukaa kwa miezi bila serikali muda ambao Macron alikuwa anataka kuutumia ili awe na mwelekeo mmoja na Merkel katika mpango wake wa mageuzi ya Ulaya.

Lazima mapendekezo ya Macron yaangaliwe iwapo yanaizingatia Ujerumani

Lakini Merkel ana sababu nyengine za kujitenga na mpango huo. Mawazo ya Macron yanahusu kupangwa upya kwa muungano wa kifedha ikiwemo kuwepo kwa bajeti ya Ulaya na kubuniwe afisi ya Waziri wa Fedha wa umoja huo. Lakini Merkel anapata shinikizo kutoka kwa Wahafidhina bungeni asikubali mageuzi yoyote ambayo yatawabebesha mzigo mkubwa zaidi walipakodi wa Ujerumani.

Joachim Pfeiffer MdB CDU
Mwanasiasa wa Kamati ya Kiuchumu wa CDu Joachim PfeifferPicha: Deutscher Bundestag/Lichtblick/Achim Melde

Mwanasiasa wa kamati ya kiuchumi ya CDU Joachim Pfeiffer amesema, "kwanza kabisa  ni sharti tuangalie iwapo mapendekezo ya Macron yanaizingatia Ujerumani pia." Naye mwansiasa wa chama cha CSU Alexander Dobrindt amekataa wazo la Waziri wa Fedha wa Ulaya akisema hilo si suala la kujadiliwa sasa.

Msemaji wa mambo ya nje wa CDU Norbert Röttgen amesema vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU havitomuwekea mipaka Merkel katika mazungumzo yake na rais huyo wa Ufaransa.

Kusita sita kwa vyama vya CDU na CSU hakukifurahishi chama cha SPD ambacho kiko kwenye serikali ya muungano na Wahafidhina hao. Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema, "tunaishi wakati ambapo tunaihitaji sana Ulaya."

Chama cha Kijani hakiridhishwi na mgawanyiko wa serikali kuhusu suala hilo la Macron

Lakini Maas anawafahamu wakosoaji wa Macron katika kambi yake pia wakiongozwa na Waziri wa Fedha Olaf Scholz ambaye hajaonesha kuridhishwa na mapendekezo ya mabadiliko ya kifedha ya rais huyo wa Ufaransa.

Belgien Deutscher Außenminister Heiko Maas
Mwanasiasa wa SPD Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/BELGA/N. Maeterlinck

Wakati huo huo mgawanyiko wa serikali ya muungano ya Ujerumani mbele ya mipango ya Macron kuhusu Ulaya ni jambo lililowaghadhabisha wapinzani wa chama cha Kijani. Anton Hofreiter ni kiongozi wa chama hicho na ametoa wito kwa Kansela Merkel na viongozi wa vyama vya CDU na CSU pamoja na SPD wampe Macron ahadi muhimu wiki hii. Hofreiter ameongeza kwa kusema mradi wa kihistoria wa Ulaya haustahili kufeli kwasababu ya ubinafsi wa serikali na mambo madogo madogo ya kisiasa ya vyama.

Mradi wa Macron hautokwenda mbali bila uungaji mkono wa Ujerumani lakini Rais wa Halmashauri Kuu la Ulaya Jean-Claude Juncker alimuonya Macron kwamba Ulaya si Ufaransa na Ujerumani pekee.

Mwandishi: Maximiliane Koschyk

Tafsiri: Jacob Safari/Tableau/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga