1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kuwashinda Dola la Kiislamu kwataka umoja

Alexander Kudascheff/Mohammed Khelef8 Septemba 2014

Huku mataifa ya Magharibi yakikabiliana na kundi linalojiita "Dola la Kiislamu", mhariri mkuu wa Deutsche Welle, Alexander Kudascheff, anasema kinachohitajika ni mkakati wa kijeshi na kisiasa.

https://p.dw.com/p/1D8qi
Wapiganaji wa kundi linalojiita "Dola la Kiislamu."
Wapiganaji wa kundi linalojiita "Dola la Kiislamu."Picha: picture-alliance/AP Photo

Sio tu kwamba ni lazima kundi la "Dola la Kiislamu" lidhibitiwe lakini pia liangamizwe kabisa, kwanza kijeshi na kisha kisiasa kwa kuvunja mazingira yanayokuza upotoshaji wao wa vita vitakatifu vya jihadi. Yumkini hayo ndiyo matarajio ya Marekani na ulimwengu mzima wa Magharibi.

Tayari Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeanzisha muungano wa mataifa kumi yaliyo na dhamira ya kupambana na "Dola la Kiislamu" – ikiwemo Ujerumani, lakini kile kinachotakikana hadi sasa ni dhamira ya kisiasa kusindikiza kampeni hiyo ya kijeshi.

Bila ushirikiano, "Dola la Kiislamu" hawatashindwa

Kilicho wazi kabisa ni kitu kimoja: vita dhidi ya "Dola la Kiislamu" haviwezi kupiganwa na mataifa ya Magharibi pekee, bali kwa kuwa na washirika kutoka eneo hilo. Endapo Marekani ikifanya hili pekee, au hata pamoja na Uingereza, propaganda itasambazwa haraka kwamba hivyo ni "Vita vya Msalaba".

Kwa hivyo, panahitajika washirika kwenye eneo hilo, ambao kwanza kabisa ni Iraq na serikali yake. Lakini jeshi la Iraq ni dhaifu na limepoteza morali ya kupigana.

Mhariri Mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.
Mhariri Mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.Picha: DW

Vile vile, serikali kuu mjini Baghdad ina wapinzani wengi: makabila ya Kisunni na wale wanaoendelea kukitumikia chama cha zamani cha Saddam Hussein, Ba'ath, chini kwa chini. Kwa hivyo, serikali kuu itajikuta ikipigana vita viwili, jambo ambalo hailiwezi.

Mshirika mwengine muhimu kwenye vita dhidi ya waasi wa "Dola la Kiislamu" yupo Damascus: Rais Bashar al-Assad wa Syria ambaye mataifa ya Magharibi yamekuwa yakimpuuza.

Kushirikiana kunaweza kuonekana jambo lisilofikirika, lakini bila ya Assad, waasi wa "Dola la Kiislamu" hawawezi kushindwa. Hii ni njozi kwelikweli kisiasa, kwani inayafanya mataifa ya Magharibi yaliyotaka muda mrefu kumuangusha Assad, kuhitaji msaada wake, lakini ni siasa halisi ambazo haziepukiki.

Mshirika wa nusu imani

Mshirika wa tatu ni Wakurdi, ambao tayari wameshaanza kupewa silaha. Lakini – kama ambavyo ungekisia – ni kwamba wakishinda, hamu yao ya kuwa na dola huru itakuja juu, jambo ambalo hakuna hata mmoja anayelitaka.

Na mwisho kuna Iran, ambayo bado inajizuia lakini itaingilia kati endapo jamii ya Kishia nchini Iraq itakuwa kwenye matatizo ya kikweli, ama inakaribia kushindwa au maeneo matukufu ya Kishia mjini Karbala yakihatarishiwa usalama wake.

Na ziko wapi nchi za Kiarabu? Misri, Jordan, Saudi Arabia. Kwao wao ni jambo lisilomezeka kupambana ama upande wa Assad au Mashia wa Iraq, kwa hivyo wamejitenga kando. Yumkini wasiweze hata kuwashambulia maadui kwenye mipaka ya nchi zao wenyewe.

Juu ya yote hayo, “Dola la Kiislamu” ni kundi linaloweza tu kukabiliwa na muungano mkubwa wa mataifa na mirengo ya kisiasa kuweza kumshinda mwendawazimu mwenye siasa kali, Abu Bakr al-Baghdadi.

Hakuna mtu anayetaka ukatili wa nyakati za kabla ya Uislamu na unaopingana na Uislamu wenyewe. Vita dhidi ya nadharia ya jihadi ni vita vya haki kwa wale wote wanaotaka Mashariki ya Kati liendelee kuwa eneo ambalo Waislamu, Wakristo na wa imani nyengine wanaishi pamoja.

Mwandishi: Alexander Kudascheff
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf