1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kuangushwa ndege ya Urusi kumesababisha mvutano

25 Novemba 2015

Kitendo cha Uturuki kutungua ndege ya Urusi kitazitatiza juhudi za Rais wa Ufaransa Francois Hollande za kuujenga mfungamano dhidi ya magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu, asema Miodrag Soric wa DW.

https://p.dw.com/p/1HCCy
Ndege ya kivita ya Urusi
Picha: Reuters/S. Zhumatov

Kadhia ya kutunguliwa ndege hiyo itazitatiza juhudi za Rais Hollande pia kutokana na ukweli kwamba Ufaransa haina uzito mkubwa sana wa kisiasa.Mkasa huo umesababishwa kana kwamba hakuna matatizo ya kutosha.

Msimamo rasmi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO ni kusimama pamoja na mshirika wake,Uturuki. Na siyo tu Nato, bali Marekani na Ufaransa pia zimeusisitiza msimamo huo kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi hizo:viongozi wa nchi hizo wameisitiza kwamba Uturuki ina haki ya kuilinda anga yake.

Lakini katika upande mwingine, Uturuki itapaswa kuwa tayari kuvutwa sikio.Kadhia ya kuangushwa ndege ya Urusi inaweza kuchochea mvutano usiokuwa wa lazima.

Mwandishi wa maoni Soric Miodrag
Mwandishi wa maoni Soric Miodrag

Mambo yanakuwa magumu wakati ambapo Rais wa Ufaransa Hollande anatarajiwa kufanya ziara nchini Urusi kwa lengo la kumshawishi Rais Putin aache kumuunga mkono Rais wa Syria Bashar al- Assad.

Hata hivyo Urusi pia inabeba sehemu ya lawama juu ya hali ya sasa.Inachukua hatua kivyake nchini Syria.Hilo ni jambo la hatari.

Ziara ya Hollande nchini Urusi itakuwa ngumu

Mvutano uliosababishwa na kadhia ya ndege ya Urusi, iliyoangushwa, haupaswi kukuzwa, la sivyo watakaonufaika watakuwa magaidi wa dola la kiislamu .Ziara ya Rais Hollande nchini Urusi haitakuwa rahisi kutokana na mkasa wa ndege hiyo.Hata hivyo juhudi zake za kuujenga mfungamano wa kimataifa, ikiwa pamoja na Urusi na Iran, dhidi ya magaidi wa dola la kiislamu zinastahili kupongezwa.

Lakini inapasa kutilia maanani kwamba Ufaransa haina uzito mkubwa wa kisiasa duniani, na sambamba na ukweli huo, nchi za Ulaya zimegawanyika, kama inavyokuwa wakati wote na hazitaki kutumia fedha kwa ajili ya mahitaji ya kijeshi.

Marekani ndiyo nchi pekee yenye nguvu za kuweza kuujenga mfungamano wa nchi zote dhidi ya magaidi wanaoitwa dola la kiislamu

Marekani inao uzito wa kuikaripia Uturuki. Marekani pia inaweza kuitambua Urusi kuwa muhimu katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Syria. Aidha Marekani inao uzito wa kuzishinikiza Saudi Arabia na Umoja wa Falme za kiarabu zifanye mazungumzo na mwakilishi wa Rais Assad. Suluhisho la mgogoro wa Syria litaweza kuletwa ikiwa pande zote zitashirikishwa.

Mwandishi: Miodrag Soric

Mfasiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman