Maoni: Kizazi kijacho kulipa madeni ya janga la COVID-19
28 Mei 2020Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amechukua hatua ya kijasiri katika bajeti kabambe ya miaka saba ijayo aliyoipendekeza. Tutaona ni vipengele gani vya bajeti hiyo vitakavyosalia baada ya nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuipitia. Bajeti hii yenye mchanganyiko wa mifuko ya uokozi na bajeti ya kuleta mabadiliko inatakiwa kupitishwa na wanachama wote bila pingamizi. Kutakuwa na mijadala mikali katika wiki zijazo, hasa kuhusu nani atapewa kiasi gani na kwa masharti yapi.
Ursula von der Leyen anadai kwamba alijadili mpango huu unaohitajika haraka na serikali zote na kwamba hakukutana na pingamizi kali. Labda ni kwasababu wanachama wa Umoja wa Ulaya wamegundua ujanja wa kuepuka kuwatwika walipakodi wa leo mzigo wa kurejesha madeni haya, na badala yake mzigo unaviangukia vizazi vijavyo. Umoja wa Ulaya unataka kukopa Euro bilioni 750. Deni litaanza kurejeshwa mwaka 2028 na litarejeshwa kidogo kidogo kwa kipindi cha hadi miaka 30 ijayo.
Ili kukusanya fedha ya kutosha kwa ajili ya kuanza kurejesha deni kuanzia mwaka 2028 na kuendelea, von der Leyen anapendekeza kutoza kodi kwenye bidhaa za plastiki, kwenye utoaji wa gesi ya carbon di oxide na pia kwenye bidhaa zinazoharibu mazingira zinazoagizwa kutoka nchi zizsizo mwanachama. Kwa mtazamo wa sera za fedha, mpango huu ni kama ndoto tu. Mwisho wa siku, nchi wanachama ndizo zitakazolazimika kurejesha madeni hayo. Kwa maana hiyo, ni walipakodi wa Ulaya watakaolipa.
Umoja wa Ulaya useme ukweli kuhusu kurejesha deni
Inawezekana pia kuwa mpango uliopo si kurejesha deni ambalo Umoja wa Ulaya umejitwisha kwa mara ya kwanza. Labda mpango ni kulisogeza na kulisogeza, kama ilivyo kawaida kwa mataifa kufanya. Mpango wa madeni uliopo sasa ni suluhu nzuri kwa nchi mwanachama kwani inamaanisha kuwa mzigo wa deni hautazilemea bajeti zao za kitaifa.
Kwa hiyo tatizo limehamishiwa kwenye siku zijazo. Kutokana na msukosuko wa kiuchumi uliosababishwa na juhudi za kupambana na janga la virusi vya corona, inaeleweka kwanini Umoja wa Ulaya unafikiria kuchukua suluhu hii. Lakini Halmashauri Kuu na nchi wanachama zinatakiwa kuwa wakweli kuhusu wanachokifanya, badala ya kudanganya kwamba madeni yanaweza kulipwa na aina ya kodi.
Madeni yataleta mshikamano
Kwa njia hiyo, jina ambalo Urusla von der Leyen ametoa kwa mpango wake wa kiuchumi, ambalo ni: „Umoja wa Ulaya wa Kizazi KIjacho", litakuwa na maana zaidi. Ni kizazi kijacho cha Ulaya kitakacholipa janga la leo. Pamoja na pungufu za bajeti za mabillioni ya Euro, watoto wanabebeshwa madeni ya Umoja wa Ulaya pia. Wakiwa na bahati labda kutakuwa na uwekezaji wa maana.
Hata hivyo, hakuna jambo zuri zaidi ambalo lingeweza kuutokea Umoja wa Ulaya. Kwasababu madeni yanawaunganisha watu na mataifa pamoja. Kujitoa kwenye muungano huu katika siku zijazo litakuwa jambo ambalo litakuwa vigumu sana kufanya na itakuwa hatua ya ghali sana. Kwa namna hiyo, Umoja wa Ulaya una kitu kama garantii ya uwepo wake kuendelea kudumu.
Soma Zaidi: Maoni: Mwendokasi wa hatifungani za Korona
Mashirika: DW