Maoni juu ya matokeo ya uchaguzi wa jimbo la NRW
15 Mei 2017Inawezekana kuwa matokeo kama hayo hayataweza kuupasua ulimwengu lakini ni ushahidi wa kutosha kuwa huo ni mwenendo unaoendelea. Chama cha Christian Democratic Union (CDU) kimeutwaa ushindi, chama cha Social Democratic Union (SPD) kinaugulia kushindwa na chama cha Walibelari cha FDP kinafurahia kufufuka kwake upya. Jambo lililoweza kutabirika mapema katika siasa za jimbo hilo la North Rhein - Westphalia ni juu ya chama kinachojiita cha siasa mbadala kwa Ujerumani cha AfD kupata kwake mafanikio madogo kwenye uchaguzi wa jimbo uliomalizika pia si ajabu vilevile kuuona ushawishi wa chama cha Kijani ukididimia.
Kwa jumla wapiga kura wameonyesha upeo wao wa kutaka utulivu katika siasa. Ukweli utabaki kuwa chama cha CDU kimeshinda jimbo kubwa la North Rhein Westphalia ikiwa ni kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Ushindi huo ukiongozwa na Armin Laschet ambaye si mtu mwenye hamasa sana lakini sifa alizojikusanyia katika kampeni zake ni kwamba yeye ni mtu mzuri.
Swali linalojitokeza kwa sasa ni je aliunyakuaje ushindi huo? Kuna majibu mawili hapa, kwanza uchaguzi wa jimbo la North Rhine - Westphalia unachukuliwa kama kipima joto cha uchaguzi mkuu ujao wa Septemba hapa nchini Ujerumani, na pili
haijalishi tena kuwa imebakia miezi minne tu hadi hapo uchaguzi mkuu utakapofanyika na kwamba juhudi za kansela Angela Merkel zinajionyesha wazi ukizingatia ushindi wa chama chake cha CDU katika maeneo ya Rhine na Ruhr na itakuwa haikidhi haja kufikiria vinginevyo tofauti na ukweli huo uliopo.
Katika wiki zilizopita hisia za kisiasa zilibadilika katika jimbo zima la NRW na maswala yaliyotiliwa maanani zaidi yalikuwa ni kubadilishwa mfumo wa madarasa katika elimu, swala la usalama pia kuongezeka kwa visa vya uhalifu pamoja na ongezeko la msongamano wa magari. Hata hivyo wapiga kura waliangalia zaidi maswala ya kimataifa katika kufanya maamuzi yao kwenye upigaji kura mwaka huu katika jimbo la NRW ikiwa ni pamoja na hali taabani ya Umoja wa Ulaya ambayo imesababishwa na hatua ya Uingereza ya kutaka kujiondoa kwenye umoja huo maarufu kama - Brexit vilevile siasa za zinazolemea mrengo mkali wa kulia katika nchi za Poland, Hungary, Austria, Ufaransa na utawala wa rais wa Marekani Donald Trump ambao kwa wengi hauna uhakika. Haijawahi kutokea uchaguzi wa jimbo kugubikwa katika maswala ya kimataifa kama uchaguzi wa wakati huu uliomalizika.
Kansela Merkel sasa anaungwa mkono na wapiga kura wengi ambao kwa kawaida wangelivipigia kura vyama vingine ijapokuwa uungwaji mkono kutoka ndani ya chama chake cha CDU umepungua kidogo. Kumekuwa na chaguzi tatu za majimbo mwaka huu na chama cha CDU kimeshinda katika chaguzi hizo zote, ushindi wa chaguzi mbili ukiwa ni katika majimbo ya upinzani. Matokeo hayo yanatoa muelekeo wa uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwezi Septemba.
Mwandishi: Zainab Aziz/Volker Wagener/ LINK: http://www.dw.com/a-38836852
Mhariri: Iddi Ssessanga