Maoni: Historia yajirudia Kenya
10 Agosti 2017Uchaguzi wa hapo Jumanne nchini Kenya ulikuwa ni wa pili kwa wagombea kutoka familia mbili zilizotawala siasa za Kenya tangu uhuru kuchuwana. Uhuru Kenyatta, mtoto wa rais wa kwanza Marehemu Mzee Jomo Kenyatta, na Raila Odinga, mtoto wa makamu wa kwanza wa Kenya, Marehemu Mzee Oginga Odinga. Uhuru na muungano wake tawala, Jubilee, wanaonekana kushinda uchaguzi huo, na kwa waziri mkuu wa zamani Raila ambaye yeye na muungano wake mpya wa kisiasa, NASA, wamepoteza, hapana shaka, hili ni pigo kubwa.
Kwake, hili tayari lilishakuwa jaribio lake la nne kuingia Ikulu, lakini kutokana na umri wake wa miaka 72, huenda ilikuwa nafasi yake ya mwisho. Hiki kilishaonekana. Odinga amewahi pia kuhoji matokeo ya uchaguzi huko nyuma, alipokwenda mahakamani na kushindwa. Kwa kuhofia kuzuka kwa mapigano, Wakenya wengi walishaona mbali.
Kwa sasa, Odinga anacheza na moto. Tayari kwenye kampeni zake, alishatangaza kwamba asingeliyatambua matokeo kama angelichezewa rafu. Sasa anayaongeza makali mapambano yake kwa kudai kwamba wadukuzi walidukua matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti. Kituo chake cha ukusanyaji matokeo, kina ushahidi kwamba yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo, tafauti na matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Isiwe kama 2007
Kauli hii inaweza kusababisha ugomvi wa kikabila na wa kisiasa. Lakini polisi nayo inapaswa kuchukuwa tahadhari katika kuyakabili maandamano. Vyombo vya usalama vya Kenya tangu hapo havina jina zuri: vinashutumiwa kwa mauaji ya makusudi, ukatili na mateso. Usiku wa kwanza baada ya uchaguzi, kuna ripoti za watu kadhaa kuuawa kutoka maeneo tafauti ya Kenya.
Asasi za kijamii, makanisa na vyombo vya habari vimetoa wito wa amani kabla na baada ya uchaguzi. Bado Wakenya wana mshituko wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na mamia kwa maelfu ya wengine kuhamishwa makaazi yao. Hili halipaswi kutokea tena!
Lakini duniani kote, kuna wasiwasi juu ya uwezekano wa ghasia mpya kuzuka: Barack Obama, ambaye baba yake anatokea Kenya, aliwageukia Wakenya na kuwaomba wasielekee huko. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alishatoa wito wa kuwepo kwa Amani.
Sasa ni wakati wa Odinga, anayependa kujionesha kama kiongozi mwanademokrasia, kufanya hivyo hivyo. Hapaswi kuwachochea wafuasi wake zaidi, bali kuchaguwa njia sahihi, ambayo ni kuitaka mahakama kuthibitisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi.
Katika siasa za kieneo, ni muhimu kwa Kenya kubakia na amani. Nchi hiyo inatajwa kuwa ngome ya vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabaab kutoka Somalia. Mataifa ya Afrika Mashariki, kama Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini yanaitegemea Kenya kusafirishia bidhaa muhimu, ndio maana kuna msemo: "Kenya ikipiga chafya, eneo zima huugua mafua!"
Kibarua kwa Kenyatta
Na Kenyatta je? Katika kipindi cha kwanza cha muhula wake, aliendeleza miradi mingi ya miundombinu na umeme nchini Kenya. Kwa sasa nchi hiyo ina ukuwaji wa uchumi wa takribani asilimia 6. Lakini wakati huo huo, ofisi yake inatajwa kutopea kwenye kashfa ya kifisadi, huku pengo baina ya masikini na matajiri likizidi kuwa kubwa.
Kwa hivyo, milionea Kenyatta ana mengi zaidi ya kuyafanya: kuunda nafasi za ajira kwa taifa ambalo wakaazi wake wengi ni vijana, kuhakikisha kuwa ukuwaji wa uchumi unawafaidisha watu wengi zaidi, kuifanya bei ya chakula kuwa nzuri na kupambana na ufisadi unaoongezeka.
Ama ikiwa anataka kuifanya kazi hii kwa umakini, ni jambo linalozusha maswali – kwa sababu tayari alishapata kipindi kizima cha kufanya hayo.
Kwa upande mwengine, inatazamiwa kuwa Wakenya watabadilisha mfumo wao wa uchaguzi unaojikita kwenye makabila, na kuanzisha tabaka jipya la kisiasa lenye vijana na lisilo na dhana mbaya baina yao. Hao wawe ni wanasiasa walio makini na ahadi zao na wanaozitekeleza kwa manufaa ya watu wote.
Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga