Maoni: China yatumia chanjo ya corona kutanuwa ushawishi
2 Februari 2021Wakati janga la virusi vya corona lilipoipiga Ulaya mwaka Uliopita, rais wa serbia Alexander Vucic alianza kwa kulipuuza. Lakini baada ya kugundua lilikuwa la kutisha, alianzisha hatua za kufunga shughuli na zilizokuwa ni ngumu zaidi kuliko mahala popote Ulaya. Miezi michache baadaye alitangaza kuvishinda vita dhidi ya janga hilo.
Rais wa Serbia kwa mara nyingine amechukua hatua za kukabiliana na COVID-19, na serikali yake inahakikisha kwamba kila mmoja anazieleewa hatua hizo. Lakini pia huwakumbusha watu kwamba Serbia inafanya vizuri kuliko mataifa mengine yote ya Ulaya.
Ukitembelea mji mkuu wa Serbia unaweza kudhani kwamba kila kitu kipo sawa, kwamba Serbia imeachana na hatua za kupambana na janga hilo. Mikahawa iko wazi na biashara zinaendelea kama kawaida. Watu wanaendelea kufurika kwenye majengo ya maduka. Wengi miongoni mwao wanaonekana ni kama wamesahau barakoa zao. Na hata wale waliozivaa basi wanazivaa kimakosa, na pua zao ziko wazi kabisa.
Mamilioni ya dozi za chanjo yaliyoingizwa kutoka China pamoja na ahadi ya chanjo nyingine kutoka Urusi vimeimarisha imani ya Waserbia wengi. Hisia kama hizo, zinajitokeza pia kwa kiongozi huyo ambaye amekuwa mwepesi kuwaambia watu mafanikio yake katika vita dhidi ya COVID-19.
Anajitanabahisha kama mlinzi wa watu wa Serbia, kiongozi wa umma asiye mbinafsi na anayefanya kazi muda wote ili kuhakikisha anapata kiasi cha kutosha cha chanjo.
Lakini hata hivyo, mtindo na matamshi yake havina ukweli, achilia mbali kwamba hayafai hata kidogo. Anazungumzia "vita" vilivyopo miongoni mwa mataifa vya kupata kiasi cha kutosha cha chanjo dhidi ya virusi vya corona. Kwa kufanya hivyo, lengo lake linaonekana ni kujinasibu tu kama shujaa kwa watu wake.
Serbia haina sababu yoyote ya kujiweka mbele hasa kwa kuzingatia kwamba mfumo wake wa afya unakabiliwa na hali ngumu, huku wengi wakimtaja rais huyo kuwa tatizo la msingi. Hawana imani na takwimu za maambukizi zinazotolewa.
Chanjo kutoka Urusi na China hazijpata kibali kutoka kwa mamlaka ya usimamizi kwenye mataifa ya Magharibi, na kuongeza changamoto kwa serikali za mataifa hayo, hatua itakayochangia kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watu wake, lakini pia serikali zikikabiliwa na shinikizo la kupeleka chanjo kwa watu wake.
Lakini hata hivyo hili halitaweza kutokea ndani ya Umoja wa Ulaya. Mshikamano ndani ya umoja huo si suala la mjadala. Ujerumani, ambayo ni taifa mwanachama tajiri na mkubwa zaidi haitaweza kuyaacha mataifa mengine madogo ya umoja huo kubaki nyuma.
Serbia si mwanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini kwa pamoja na mataifa ya Balkani magharibi, imepata mamilioni kutoka kwa Brussels ili kukabiliana na janga hilo. Hata hivyo, Belgrade inalipuuza hilo.
Mtu anaweza kuwa mjinga kufikiri kwamba chanjo kutoka China, zinakuja bila ya masharti yoyote, kwamba zinaletwa tu kwa sababu ya ubinaadamu ama labda inaomba radhi kwa sababu gonjwa hilo lilianzia huko.
China ni taifa linalofikiria maslahi ya muda mrefu. Wakati likikabiliwa na changamoto za kujiingiza kwenye makampuni ya Ujerumani, Uingereza na Marekani, inaweza kufanya chochote ambacho ni kirahisi kwake na kisicho na gharama kwenye mataifa kama Serbia ama Hungary. Na kwa kufanya hivyo, mataifa hayo yanakuwa tegemezi kwa China sio tu kiuchumi bali pia kisiasa, kama ilivyokuwa kwa Amerika ya Kusini na Afrika.
Itakuwa ni kosa kubwa la kimkakati iwapo mataifa ya magharibi yataruhusu Urusi na China kuimarisha ushawishi wake katika maeneo la Balkani magharibi. Angalau basi, hata Umoja huo ungeunga mkono juhudi za Montenegro za kujiunga nao. Watu nchini humo tayari wameachana na sehemu ya historia ya kikomunisti.
Iwapo lengo la Umoja wa Ulaya ni kuonyesha kwamba demokrasia ndio mlango wa mafanikio ya kikanda, basi Montenegro ni mahapekee ambapo unaweza kuipigia debe hoja hiyo.