Maoni: Buhari aachie ngazi
3 Mei 2017Ni kwa bahati mbaya kwamba rais wa Nigeria amekuwa mgonjwa na kwa nyakati tofauti hakuweza kushiriki katika masuala muhimu yanayowoathiri wananchi wa kawaida. Mnamo mwezi Machi alirejea kutoka jijini London ambako alitumia wiki karibu saba akipatiwa matibabu. Mwishoni mwa mwezi wa nne alishindwa kuhudhuria mkutano wa pili wa baraza lake la mawaziri kwa mfululizo katikati mwa uvumi juu ya hali ya afya yake. Wanigeria wanaelewa vyema madhara ya kumpoteza rais aliyeko madarakani kuliko mtu yoyote yule.
Kifo kisichotarajiwa cha rais Umaru Yar'dua mwaka 2010 kilichochea mvutano wa kisiasa kabla ya kumuapisha rais Goodluck Jonathan, mtangulizi wa Buhari. Buhari aliye na miaka 74, amekuwa madarakani kwa miaka miwili pekee. Mafanikio aliyoyapata ndani ya kipindi hicho kifupi yanatosha kujieleza yenyewe. Amepambana na kulidhoofisha kundi la wanamgambo la Boko Haram, suala ambalo mtangulizi wake Jonathan alishindwa kulifanya.
Buhari kiongozi wa zamani wa kijeshi, pia alizidisha mapambano dhidi ya rushwa. Aliiongezea nguvu kamisheni ya makosa ya kiuchumi na kifedha ya EFCC ambayo nayo haikusita bila hofu kufanya uchunguzi na kuwakamata maafisa wa zamani waandamizi ambao walikuwa hapo awali hawaguswi.
Ushindi wa Buhari ulikuwa ishara nzuri
Kuchaguliwa kwa Buhari mwezi Machi 2015 dhidi ya rais aliyekuwa madarakani Jonathan kuliwashangaza Waafrika wengi. Ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria ambapo rais aliyekuwa madarakani kupoteza kwa mgombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu. Pia iliongeza matumaini kwa waafrika wengi kwamba hatimaye katika bara, madaraka yanaweza kupatikana bila ya umwagaji damu.
Katika sehemu nyingi za Afrika upinzani umekuwa dhaifu kuweza kumwondoa madarakani rais kupitia mchakato wa kidemokrasia na ulio wazi wa uchaguzi. Viongozi wa kimabavu mara kadhaa wamekuwa wakidhoofisha sauti za upinzani kupitia ukandamizaji wa kisiasa wakati wakitumia rasilimali za taifa kwa kuruhusu upendeleo.
Ushindi wa Buhari umewaimarisha wengi Afrika Magharibi. Rais wa Ghana Nana Akufo Ado ambaye alikuwa ni kiongozi wa upinzani, alifanikiwa kumwondoa rais John Mahama mwezi Desemba mwaka jana katika uchaguzi mkuu. Mahama alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa nchini Ghana kupoteza uchaguzi baada ya kipindi cha kwanza madarakani.
Huko Sao Tome na Principe, Evaristo Carvalho alimshinda rais Manuel Pinto da Costa ambaye amekuwa rais kati ya mwaka 1975-1991 na 2011-2016. Hata hivo, matokeo yatakayokumbukwa kwa miaka kadhaa ni ya kuhusu Gambia ambako rais Yahya Jammeh aliyeingia madarakani na kudumu kwa miaka 22 kupitia mapinduzi aliangushwa na mgombea aliyekuwa akiwakilisha muungano wa upinzani Adama Barrow. Jammeh aliyeko uhamishoni kwa hivi sasa mwanzoni alionekana kumeza machungu ya kuangushwa kwake lakini baadae akashindwa kuyatafuna.
Hakuna rais anayetakiwa kuongoza akiwa kwenye kiti cha walemavu
Alikataa kukubaliana na matokeo hayo na hivyo kupata shinikizo la kisiasa na kijeshi kutoka kwa rais Buhari na viongozi wengine wa nchi wanachama wa jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ECOWAS. Mafanikio haya ya kisiasa angalau kwa Afrika Magharibi yanapaswa kuimarishwa na kulindwa.
Kuugua kwa Buhari bado kunachukuliwa kama suala la binafsi hata kama ni mtu aliye na nyadhifa ya juu serikalini. Baadhi ya watu wanasema aliingia madarakani wakati akifahamu fika kwamba asingeweza kumudu kazi hiyo. Kukosekana kwa utamaduni wa kuhoji juu ya viongozi wa afrika kunadhoofisha maendeleo kadhaa yaliyopatikana. Afya za viongozi wa umma kama Buhari ni suala linalogusa maslahi ya umma na linapaswa kuchunguzwa kwa ukaribu.
Rais Buhari amejizolea heshima kwa mafanikio aliyoyapata ndani ya muda mfupi. Anachohitajika kwa hivi sasa ni kuwa mwangalifu na afya yake na kuacha masuala ya kitaifa mikononi mwa wenzake. Nina uhakika kwamba mwenyezi Mungu amewahifadhi wengi kiafya, viongozi wasio na kashfa za rushwa na wenye haiba kubwa ya uongozi ambao wanaweza kuchukua kutoka kwake. Ni katika maslahi ya Wanigeria kwamba rais Buhari aachie madaraka.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Fred Muvunyi
Mhariri: Josephat Charo