Maoni: Baada ya mahaba kwa Schulz, sasa ni kazi kwenda mbele
20 Machi 2017Ni jambo la kawaida kuwa na furaha kubwa katika mkutano mkuu wa chama pale kiongozi mpya anapochaguliwa. Lakini mkutano usio wa kawaida wa chama cha SPD ambako Martin Schulz alichaguliwa rasmi kuwa mwenyekiti wa chama na mgombea wa ukansela ulikuwa tofauti.
Furaha ya wajumbe 2,500 pamoja na wageni ilikuwa ya kweli, shauku yao isiozuwilika ilikuwa inaonekana dhahiri. Shulz ndiye kiongozi wa kwanza wa SPD kuchaguliwa kwa asilimia 100, bila hata kura moja ya kumkataa.
Kwa upande mmoja ni jambo zuri kwamba siasa inaweza kuwasisimua watu namna hii. Lakini jambo hili linahusu siasa kweli? maudhui au Hoja? Martin Schulz hajatimiza yote hayo mpaka sasa, na yumkini ikachukuwa miezi mingine mitatu kabla hajawasilisha ilani ya uchaguzi -- wanasema mwezi Juni.
Hadi wakati huo, lipo tu pendekezo la kuazisha kitu kinachoitwa "mafao ya wasio na ajira Q," ambayo yatatoa motisha ya kifedha kwa watu kupata mafunzo zaidi. Ingawa kuna sababu ya kujiuliza namna hilo linavyosaidia katika wakati ambapo kuna nafasi nyingi za kazi zinazojitokeza, lakini hilo siyo lengo la wakati huu.
Fahari na mapenzi
Kwa sasa suala siyo kuhusu ukweli, ilani, au juhudi kwa ngazi ya kisiasa. Ni kuhusu viashiria, makadirio na matarajio. Martin Schulz anavutia hisia za watu; anafanya hivyo kwa ustadi mkubwa na vema. Ameingia katika ombwe la hisia, na inaonekana anao uwezo wa kufufua kwa urahisi, mapenzi na fahari ambavyo SPD imevipoteza katika miaka ya karibuni.
Na ndiyo maana kitu cha kwanza alichofanya ni kujitenga na Agenda 2010, ambao ni mpango wa mageuzi uliopitishwa na SPD zaidi ya miaka kumi iliopita, lakini ambao bado unawachefua wanachama wengi mpaka leo hii. Programu ya ustawi ya Hartz IV, malipo ya wasio na ajira yalioboreshwa na mambo mengine yalioambatana na mpango huo bado vinachukuliwa na wengi ndani ya SPD kama usaliti wa maadili yao ya msingi wa kijamii.
Ikiwa Martin analenga kubadili kitu -- yaani kitu chochote -- hilo pekee ni jambo la kuliwaza kwa wana SPD. Ni mwanga wa matumaini -- matumaini kwamba uongozi wa kisiasa utakirejesha chama kwa dhamira yake kuu ya "haki," na hivyo kukirejeshea heshima yake ya zamani. Heshima kiliokuwa nayo SPD chini ya Willy Brandt.
Mapendezi kuendelea hadi Septemba?
Matukio ya karibuni yamechochea zaidi hisi hizi. Maelfu wamerejea SPD, na wapya wamejiunga, umaarufu wa SPD umeongezeka katika uchunguzi wa maoni. Na Schulz anaonekana kweli kama chaguo mbadala kwa Merkel. Lakini swali kubwa ni je, ni kwa muda gani Schulz ataendelea kuwa kivutio na mwanga wa matumaini kwa SPD?
Kwa kuwa Schulz siyo mwanachama wa bunge la shirikisho, halaazimiki kujihadhari na mambo nyeti yanayohusu muungano mkuu kati ya SPD na vyama vya CDU na CSU. Anaweza kushambulia, na kujijengea sifa. Anao uhuru wa kisiasa ambao wengine hawana, na hilo linampa faida.
Anachotakiwa kufanya sasa ni kuutumia uhuru huo kikamilifu. Njia alioshika inaonekana kuwa sahihi. Shauku ya kuwa na ulimwengu wa haki, usalama na uaminifu imekuwa kubwa zaidi kuliko kabla. Ikiwa Martin Schulz hatofanya makosa mengi katika kipindi cha miezi sita ijayo, basi anayo fursa kubwa ya kuongoza katika uchaguzi wa Septemba 24.
Mwandishi: Sabine Kinkartz
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba