Maoni: Afrika yapiga hatua
2 Februari 2015Bila shaka viongozi wengi waliohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika walizikumbukia enzi za dikteta Muamar Ghaddafi ambaye alijitapa kuwa mfalme wa wafalme wa Afrika. Hawakumkumbuka kwa sababu ya misemo kama hiyo bali zaidi kwa sababu ya kitita cha fedha ambacho kilikuwa kinatoka kwenye serikali yake kuufadhili Umoja wa Afrika.
Lakini sasa Umoja wa Afrika unakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na tunashuhudia kuwa wakuu wa Umoja huo wanaonyesha ubunifu mkubwa linapokuja suala la kutafuta mapato: Wamekubaliana kutoza kodi kwa tiketi za ndege, malazi hotelini na pia huduma za sms. Kwa namna hiyo inatarajiwa kwamba AU, ndani ya mwaka mmoja, itajipatia dola za Kimarekani bilioni 2.5 - kiasi kinachotosha kabisa kugharimia wanajeshi wa kulinda amani na juhudi za kupambana na Ebola. Kiasi hiki ni sawa na theluthi mbili za bajeti ya AU kwa mwaka 2016. Kwa sasa Umoja huo unaweza tu kugharimia asilimia 28 ya bajeti yake.
Mugabe asiogopwe
Tatizo ni kwamba ushuru uliopendekezwa si wa lazima na tayari mataifa mengi mwanachama yanalipinga wazo hilo kwa hofu kwamba utalii na uwekezaji utarudi nyuma. Hivyo matumaini kwamba AU kweli itapata mamilioni ya pesa kupitia ushuru ni hafifu.
Pamoja na hayo, Umoja wa Afrika umepitisha uamuzi wa kutuma kikosi cha askari 7,500 wa kulinda amani kwa ajili ya kupambana na waasi wa Boko Haram Afrika Magharibi. Nigeria si nchi pekee itakayofaidika na hatua hiyo: Hata nchi jirani za Chad na Cameroon zinatamani maovu ya Boko Haram yakomeshwe haraka iwezekanavyo. Bila shaka Umoja wa Mataifa utatoa kibali kwa kikosi hiki kuanza kazi kwani ni suala linaloungwa mkono na Marekani, Ujerumani na hata Iran. Maswali mengine yanayohitaji ufumbuzi ni je, wanajeshi watatokea nchi gani na ni nani atakayewalipa?
Huenda jambo lililowafanya wachambuzi wengi wakune vichwa ni kuchaguliwa kwa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Lakini hakuna haja ya kumwogopa mkongwe huyo anayekaribia kufikisha miaka 91. AU kwa sasa ina baraza la usalama na amani linalofanya kazi barabara na ndilo linalobuni sera za kisiasa za AU. Na kwa sasa kizazi kipya cha wanasiasa wa Kiafrika kimeibuka, kizazi ambacho pia kinashangazwa na siasa za kizamani. Hizo ni habari njema kutoka Addis Ababa!
Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Saumu Yusuf