Maoni: Afrika ya Obama ni uwanja mpana
3 Julai 2013Kumalizikia nchini Tanzania kwa ziara ya Rais Obama barani Afrika kunaweza kuzingatiwa kuwa ni hatua ya maridhiano. Hata hivyo bara la Afrika bado lipo kandoni mwa ajenda ya Marekani.
Maalfu ya watu waliokuwa na furaha walimlaki Rais Obama nchini Tanzania. Kituo cha mwisho cha ziara yake ya barani Afrika kinachoweza kuzingatiwa kuwa ni hatua ya maridhiano. Huku akishangaliwa sana, Obama alitangaza alichokiita kuwa zama mpya za uhusiano na bara la Afrika. Msingi wa muundo huo mpya wa uhusiano, siyo tena misaada ya maendeleo na kuungwa mkono, bali uhusiano biashara na ushirikiano.
Dhima ya Marekani katika uhusiano mpya
Rais Obama amesema dhima ya Marekani hapo itakuwa ile ya mshirika. Hayo ni maneno mazito yaliyotoka kwa urahisi kwenye kinywa cha Obama, Rais wa kwanza wa Marekani, mwenye nasaba ya Afrika.
Mpango huo siyo wa kuliwaza sana,kiasi cha kuweza kumweka Obama katika safu moja na marais wa Marekani wa hapo awali, Bill Clinton na George Bush.Wote wawili wameingia katika historia kutokana na mipango waliyoitekeleza kwa manufaa ya bara la Afrika.
Bill Clinton alitia saini mkataba wa Agoa wa kuzipa fursa nchi za Afrika ya kuuza bidhaa nchini Marekani bila ya kutozwa ushuru. Ni mradi ambao ungeliweza kuipeleka Afrika mbali, laiti ungelitekelezwa kwa makini zaidi. Bush aliyamimina mabilioni ya fedha barani Afrika kwa ajili ya mradi wa kuwasaidia waathirika wa maradhi ya ukimwi .
Je, itahimili kishindo cha China?
Obama ametangaza kuwa Waziri wake mpya Penny Pritzer atashughulikia biashara baina ya Marekani na Afrika. Ni kweli kwamba thamani ya biashara kati ya Afrika na Marekani mnamo kipindi chama miaka 10 iliyopita iliongezeka mara mbili. Lakini biashara baina ya China na nchi za Afrika iliongezeka mara 20 katika kipindi hicho hicho.
Ni muda mrefu tokea China ilipoichukua nafasi ya Marekani kama mshirika mkubwa kabisa wa biashara na nchi za Afrika. Tuchukue mfano wa Tanzania. Biashara kati ya nchi hiyo na Marekani ilifikia thamani ya dola Milioni 360 katika mwaka uliopita. Lakini biashara baina ya Tanzania na China ilifikia thamani ya dola bilioni 2 na nusu.
Wakati Obama, katika muhula wake wa pili wa urais, alipoamua kufanya ziara barani Afrika, viongozi wa ngazi za juu wa China siku nyingi walikuwa tayari wameshalitembelea bara hilo. Rais mpya wa China Xi Jinping alikuwako nchini Tanzania mnamo mwezi wa Machi. Na kwa hivyo mambo hayatakuwa rahisi kwa waziri mpya wa biashara wa Marekani,Penny Pritzer kuitekeleza ndoto ya Obama juu ya Afrika.
Nguvu Afrika kubadilisha hali ya mambo?
Hata hivyo kijogoo kinaweza kuwika kutokana na mpango wa Marekani wa dola bilioni saba wa ugavi wa nishati ya umeme kwa nchi za Afrika unaoitwa "Nguvu Afrika." Lengo lake ni kuongeza ugavi wa umeme mara mbili kwa nchi za Afrika za kusini mwa jangwa la Sahara . Theluthi mbili ya watu wa eneo hilo hawapati huduma ya umeme. Na nchi sita ikiwa pamoja na Tanzania zimo katika hatua za mwanzo za kuunganishwa. Kaya milioni 20 zitaunganishwa katika mtandao wa huduma hiyo ya umeme.
Katika kituo cha kwanza,cha yake, nchini Senegal, Obama bado alikuwamo mnamo mkondo sahihi, angalau mwanzoni. Alienda kwenye kituo kilichotumika kwa ajili ya kuwasafirishia watumwa ng'ambo katika kisiwa cha Goree. Lakini Obama alivuruga mambo aliposositiza juu ya haki za mashoga alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari na mwenyeji wake Rais Macky Sall wa Senegal.
Lakini Obama alijibiwa na mwenyeji wake kwa kwamba hakuna chuki dhidi ya mashoga nchini Senegal, lakini nchi hiyo bado haijawa tayari kuepusha kubaguliwa kwa watu hao. Ziara ya Obama , barani Afrika ilimalizika nchini Tanzania, kwa upeo wa chini kama iliyvoanza kwa Rais huyo nchini Senegal.