Maombolezi Poland kabla ya jazba ya uchaguzi
13 Aprili 2010Wananchi wa Poland, wanaomboleza wakati huu vifo vya ile ajali ya ndege ya Smolensk tena kwa njia ya huruma na maridhiano nadra kuwahi kuonekana.Wakati huo huo, wanaangalia mbele ,kwani kampeni ya jazba kubwa ya uchaguzi inawakabili.Poland, inahitaji kumchagua rais mpya,lakini pia, majibu ya maswali mengi mazito.
Ni vigumu kusema muda gani kipindi cha mapumziko kwa kampeni ya uchaguzi kitadumu.Lakini, inawezekana karibuni hivi, tukuaanza kusikia tafsiri mbali mbali za njama nyuma ya ajali iliotokea.Kwani, kitu kama hicho ni vigumu kuepuka.Hii ni kutokana na kampeni inayowakabili.
Jukumu la Rais, limechukuliwa hivi sasa kwa muujibu wa katiba na spika wa Bunge.Hatahivyo, uchaguzi wa rais ulikwisha pangwa kufanyika majira haya ya sasa.Inatarajiwa kuwa kampeni itakayojaa jazba na hamasa .
Tabaka la viongozi wa kisiasa wa Poland,litabidi kuchunga kuzuwia jazba na hamasa hizo hazivuki mpaka au kufurutu ada.Na mengi yatategemea nini viongozi wa kisiasa wa Urusi watafanya. Rais Dmitri Medwedew na waziri mkuu Wladmir Putin, hivi sasa wamepiga mfano mwema.Sio tu wanashirikiana na wapoland kupita kiasi katika kumurika nini kilichopelekea ajali hiyo,bali pia wanaonesha hata huruma na majonzi yao.Hii bila sahaka, itachangia kutuliza hamasa na jazba nchini Poland.
Juu ya hivyo, maswali magumu yanapaswa kuulizwa: Ilikuaje ,uongozi mzima wa kijeshi wa Poland pamoja na mawaziri wake 10 ukasafiri kwenye ndege moja ?
Ndege ya serikali chapa "Tuppolew 154" ni kongwe kwa zaidi ya miaka 30. Mabingwa wa ndege wakionya tangu miaka mingi kwamba, wakati umewadia wa kubadilishwa ndege hiyo .
Miaka 2 nyuma pale ndege ya rais Lech Kaczynski ilipokuwa ikielekea Japan,ndege hii hii ilibidi kutua kwa dharura nchini Mongolia. Onyo pia hapo lilitolewa kwa hatari ya kusafiri na chombo hicho.Wakati ule hakuna aliepozea maisha.
Miezi 2 iliopita, ndege hii, ilifanyiwa ukaguzi na ikapewa ruhusa ya kuendelea kuruka kwa miezi 3 zaidi. Kwavile, hakujagunduliwa hitilafu za kiufundi,iliobaki ni kudhania kosa lililosababisha ajali hiyo, si la kiufundi bali la mwanadamu.
Katika uwanja wa ndege wa Smolensk wakati ndege hiyo ikijaribu kutua ukungu ulitanda .Uwanja wa ndege huo unatumika zaidi kwa ndege za kijeshi.Ndege za abiria ,waongozaji kutua na kuruka ndege wa hapo hawana maarifa ya kutosha.
Kwahivyo, msiba wa Smolensk, unabainika kuwa jinamizi jengine katika historia ya Poland.Kwani, karibu tu na uwanja huo wa ndege, kuna makaburi ya wapoland, wahanga wa uhalifu wa vita uliofanywa na warusi wakati wa vita vya pili vya dunia huko Katyn.Ilikua azma ya marehemu rais Kaczynski, kuzuru juzi hapo makaburi yao.
Mwandishi: Wohlan,Hubert( DLF)
Mtayarishi: Ramadhan Ali
Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed