1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maombi ya Ugiriki ya kuongezewa muda wa kusaidiwa yakubaliwa

24 Februari 2015

Mpango wa kuisaidia Ugiriki utarefushwa .Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imetoa taarifa hiyo na kueleza kuwa msaada huo utaendelea hadi mwishoni mwezi Juni. Lakini shirika la fedha la kimataifa bado lina mashaka

https://p.dw.com/p/1Egex
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis VaroufakisPicha: Getty Images/AFP/E.Dunand

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro leo wameyakubali maombi ya Ugiriki juu ya kuongezewa muda wa kusaidiwa. Mkutano wa mawaziri hao uliofanyika kwa njia ya simu uliashiria hapo awali kupokolewa vizuri kwa maombi ya Ugiriki. Kauli ya matumaini juu ya maombi ya Ugiriki ilitolewa na Mwenyekiti wa ukanda wa sarafu ya Euro Jeroen Dijsselbloem kwenye mtandao wa Twitter.

Naye Makamu wa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema kwenye mtandao wa Twitter kwamba mpango wa kuendelea kuisaidia Ugiriki sasa unaweza kuanza. Waziri wa fedha wa Slovakia Peter Kazimir pia amesema kwenye mtandao wa Twitter kwamba makubaliano yamefikiwa na Ugiriki. Hata hivyo Waziri huyo amesema Ugiriki inayo kazi kubwa ya kuifanya hadi mwishoni mwa mwezi wa Aprili.

Jee serikali ya mrengo wa kushoto itaendelea na mageuzi nchini Ugiriki?

Serikali mpya ya Ugiriki ya mrengo wa kushoto iliyochaguliwa kutokana na kuahidi kuipinga sera ya kubana matumizi, iliyatoa maombi ya kuongezewa muda wa kuendelea kupewa mikopo, sambamba na orodha ya mageuzi ambayo Ugiriki inapaswa kuyatekeleza. Muda wa mpango wa sasa wa kuisadia Ugiriki unamaliziika Jumamosi ijayo.

Palikuwapo na wasi wasi mkubwa ,huenda Ugiriki ingeishiwa fedha kabisa na hivyo kulazimika ,kujitoa kwenye Umoja wa sarafu ya Euro endapo msaada ambao umekuwa unatolewa kwa nchi hiyo hadi sasa ungelikatika ghafla.

Mwenyekiti wa ukanda wa sarafu ya Euro Jeroen Dijsselbloem ameeleza kwamba katika maombi yake serikali ya Ugiriki imeahidi kuutekeleza wajibu wake. Amesema serikali ya Ugiriki imeahidi kujizatiti katika kuutekeleza mchakato wa kina wa mageuzi wenye lengo la kuleta ustawi wa kudumu ,kuhakikisa uthabiti katika sekta ya fedha sambamba na kuleta haki za kijamii.

Shirika la Fedha la Kimataifa bado lina mashaka

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF,Christine Lagarde ameelezea mashaka juu ya mpango wamageuzi wa Ugiriki. Mkurugenzi huyo amesema ,mpango wa Ugiriki unatosheleza kuruhusu msaada kuendelea kutolewa kwa nchi hiyo lakini mpango huo hauna habari za kina.

Katika barua aliyomwandikia Mwenyekiti wa ukanda wa sarafu ya Euro, Bibi Lagarde amesema orodha ya Ugiriki juu ya mageuzi ni kamilifu lakini haielezi kila kipengee kwa undani. Amesema katika sehemu fulani, na hasa zile muhimu sana, serikali ya Ugiriki haijatoa uhakika kwamba inadhamiria kusonga mbele na mageuzi.

Mwandishi:Mtullya Abdu.rtre,dpa,

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman