Manila. Upinzani washindwa kumshitaki rais Arroyo.
25 Julai 2005Upinzani nchini Phillippines umeshindwa katika jaribio lake la kutaka kuendesha mashtaka dhidi ya rais Gloria Macapagal Arroyo. Wabunge hawakuweza kupata uungaji mkono wa kutosha katika bunge , ili kuweza kuipeleka hoja hiyo katika kumshitaki rais katika baraza la Seneti.
Katika hotuba yake kuhusu hali ya taifa hilo, aliyoitoa mapema leo , Arroyo amekwepa kutaja suala la udanganyifu katika uchaguzi uliopita na madai ya ulaji rushwa dhidi yake.
Badala yake amelaumu mfumo wa siasa nchini humo kwa kuleta hali ya wasi wasi kisiasa inayoikumba nchi hiyo.
Katika hotuba yake kwa baraza la Congress, Arroyo amesema kuwa Philippines inapaswa kuondoa nafasi ya urais na kuingia katika mfumo wa serikali inayoongozwa na bunge.
Kiasi cha waandamanaji 40,000 walijikusanya karibu na jengo la bunge wakidai ajiuzulu.