Maneno 11 ya Kijerumani unayopaswa kuyajuwa kwa ajili ya Kombe la Dunia
Jifunze kuzungumza kama bingwa wa dunia! Wakati Kombe la Dunia likianza tarehe 14 Juni hadi 15 Julai, ni wakati wa kupiga msasa msamiati wetu wa soka - na Wajerumani wanauelezea mchezo huu kwa njia ya ubunifu kabisa.
Schwalbe
Neno hili humaanisha "mbiliwili" yaani yule ndege mashuhuri, lakini usipumbazwe na maana hiyo. Kwenye soka, "Schwalbe" ni kujiangusha kusudi kwa mchezaji baada ya ama kutoguswa kabisa au kuguswa kidogo tu na mpinzani wake, akitaka upigwe mkwaju wa adhabu. Wachezaji wanaofanya hivi mara kwa mara huitwa "Schwalbenkönig" - "wafalme wa mbiliwili."
Schiri
Hiki ni kifupisho cha neno "Schiedsrichter," linalomaanisha mtu muhimu sana kwenye mechi - muamuzi. Timu ya waamuzi ndiyo yenye dhamana ya mchezo. Ni wao wanaoamua ikiwa goli ndilo na adhabu gani inamstahikia mchezaji. Kama ilivyo kwa "Schiri", maneno mengi ya ufupisho kwenye Kijerumani hutokana na herufi au silabi ya mwanzo ya neno refu.
Fallrückzieher
Hili ni shuti la kijanja linalofahamika kama kiki ya baiskeli au upaa au mkasi. Mchezaji anakipinda kiwiliwili wake kwa nyuma hadi hewani na anarusha mguu mmoja mbele ya mwengine akiwa angani ili kuupiga mpira kurudi nyuma juu ya kichwa, bila ya kutua chini. Ni ufundi usio wa kawaida na ambao huwafanya wachezaji wanaoumudu kushangiriwa sana.
Abseits
Hili ni neno la Kijerumani kwa mchezaji anapozidi. Mchezaji anaambiwa yuko "abseits" ikiwa yuko kwenye nusu ya upande wa timu pinzani na karibu zaidi na mstari wa goli kuliko walinzi wa timu hiyo. Mchezaji akizidi, muamuzi huo mkwaju usio wa moja kwa moja kwa timu pinzani. Wakati Ujerumani itakapocheza, washangaze marafiki zako kwa kuwaonesha mchezaji aliye "abseits".
Flanke
"Krosi" ndilo neno la Kiswahili kwa "Flanke". Mbinu hii ni kuufikisha mpira kutoka kwa mchezaji kuingia kwenye eneo la hatari la timu pinzani, hasa kwa pasi ya juu. "Flanke" inamaanisha "kupembua" au "kuweka kando". Wazo ni kuufikisha mpira kwenye eneo la hatari karibu na goli - na yumkini kufunga muda mfupi baadaye.
Finte
Hii ni mbinu ya mchezaji kumbabaisha mpinzani wake aone kwamba anataka kutoa pasi au kupiga mpira, wakati lengo lake hasa ni kumpita na mpira. "Finte" inaweza ikaonekana kama pasi au shuti, au hata kutikisa kibega ili kumpa mpinzani ishara isiyo sahihi. Kwa Kiswahili inaitwa "chenga."
Notbremse
Neno hili humaanisha "breki ya dharura". Kwenye soka, hii ni ile hali ambapo mchezaji anafanya faulu ya makusudi ili kuzuwia goli la mpinzani wake. Ni mbinu hatari sana. Muamuzi akimnasa, mchezaji anapewa kadi nyekundu na mara nyingi anazuiwa mchezo ufuatao asicheze.
Elfmeter
Kila timu hufurahia inapopewa "Elmeter", yaani mkwaju wa adhabu, kwa kuwa ni njia rahisi ya kupata goli. "Elfmeter" inaweza kuamua ushindi hasa kwenye mchezo wenye ushindani mkali. Inatolewa pale faulu ya moja kwa moja inapotendeka ndani ya eneo la hatari. Mkwaju wa penalti hupigwa mita 11 kutoka golini.
Zuckerpass
Maana yake ya kawaida ni "pasi tamu". Uwanjani, hii inamaanisha pasi iliyotolewa kiwepesi, kiufundi na kibunifu. Baadhi ya pasi huwa ngumu kwa mpokeaji kuzidhibiti, lakini "pasi tamu" hutua kabisa mguuni pake. Ila si kila mchezaji bingwa anatakiwa atowe "pasi tamu" muda wote?
Tor
Neno hili linapotamkwa kwa mayowe, ambayo mara nyingi husikikana kama "TORRR!", humaanisha goli, ingawa mara nyengine hutumika kumaanisha lango. Goli huwa limefungwa pale mpira unapovuuka mstari wa goli baina ya nguzo mbili. Kama mchezaji kajifunga mwenyewe, Wajerumani huita "Eigentor."
Goldenes Tor
"Goldenes Tor" humaanisha goli pekee kwenye mechi ambayo mchezaji mmoja tu ndiye aliyetingisa wavu. Hii haina uhusiano na kanuni ya sasa ya goli la dhahabu, ambayo ina maana mbali kabisa. Kanuni hii inahusiana tu na mechi ambazo zinaingia muda wa nyongeza - na iliamuliwa kuwa goli la mwanzo kufungwa kwenye muda huo wa nyongeza ndio ambao huikamilisha mechi. Kanuni hii iliachwa mwaka 2004.