Manchester United yashinda Europa League
25 Mei 2017Paul Pogba na Henrikh Mkhitaryan walifunga bao moja kila mmoja katika kila kipindi huku timu yao, Manchester United ikiizidi nguvu Ajax Amsterdam kushinda fainali ya kombe la Ulaya, Europa League mabao 2-0 na kufuzu kwa michuano ya kombe la mabingwa barani Ulaya, Champions League, msimu ujao.
Kulikuwa na kimya cha dakika moja katika uwanja wa Friends Arena mjini Stockholm nchini Sweden kuwakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi lililofanywa na mtu wa kujitoa muhanga katika tamasha la muziki la msanii kutoka Marekani Ariana Grande mjini Manchester ambapo watu 22 waliuawa na wengine 59 kujeruhiwa Jumatatu usiku. Baadaye kabla mechi kuanza mashabiki wa Manchester United walishangilia wakipiga kelele wakisema Manchester, hatutakufa kuwakumbuka wahanga, huku Pogba pia akiomboleza kufuatia kifo cha babake Mei 12.
Paul Pogba aliifungia United bao la kwanza dakika ya 18 ya mchezo na Mkhitaryan akafunga la pili dakika ya 48, mabao ambayo yameiwezesha Manchester United kushinda kombe la Ulaya ambalo halimo katika kabati la United huko Old Trafford. Pogba amesema ushindi wao ni kwa ajili ya wahanga wa shambulizi katika ukumbi wa Manchester Arena.
"Tunafahamu vitu kama hivi vinahuzunisha sana ulimwenguni kote." Tulilazimika kutulia. Manchester - tumeshinda kwa ajili yao. Tulicheza kwa ajili ya England, tumecheza kwa ajili ya Manchester na tumecheza kwa ajili yao - watu waliokufa," akasema Pogba na kuongeza: "Lengo lilikuwa kushinda kila mechi msimu huu. Tumefaulu na tunajivunia. Watu wanasema tulikuwa na msimu mbaya lakini thawabu ni kubwa na tumefanikiwa sasa. Tuna mkombe matatu kwa hiyo furahini sasa."
Ushindi wa Manchester United umemuwezesha kocha Jose Mourinho ambaye alisema kabla mechi hiyo kwamba yeye na wachezaji walikuwa wakijitahidi kutofikiria kuhusu janga lilitokea, ili kuukamilisha msimu wake wa kwanza Old Trafford kwa ufanisi. Tayari Mourinho aliiongoza United kushinda kombe la ligi, League Cup, na licha ya kumaliza katika nafasi ya sita katika ligi ya Premier, timu yake inarejea katika mashindano ya Champions League msimu ujao.
"Huu ni mwisho wa msimu mgumu sana, lakini msimu mzuri sana." alisema Mourinho. "Kuna washairi wengi sana katika kandanda, lakini washairi hawashindi mataji mengi. Tulifahamu ni wapi tulipowazidi kwa ubora na tukatumia udhaifu wao kuwapiku," akaongeza kusema.
Mourinho amesema shambulizi la Manchester limepunguza shangwe, nderemoo na vifijo vya kushinda kombe la Ulaya na alikubalaian ana uamuzi wa UEFA kucheza fainali mjini Stockholm
"Dunia inaendelea, haisimami. Lazima tufanya kazi yetu na nilikubaliana nauamuzi wa UEFA kucheza mechi hii, lakini tunamaswali kwa mfano kuhusu mkasa huu unaotupokonya furaha ya ushindi wetu. Kama tungeweza kubadilisha kombe hili kwa maisha ya waliokufa, mara moja tungekubali, hatungefikiria mara mbili."
Manchester United ni timu ya tano baada ya Juventus, Ajax, Bayern Munich na Chelsea, kushinda kombe la mabingwa Ulaya, Champions League, kombe la ligi ya Ulaya, Europa League na kombe la UEFA Winners cup, linalowaweka pamoja washindi wa ligi ya mabingwa na ligi ya Ulaya.
Mourinho, ambaye alishinda kombe la UEFA na Porto mwaka 2003 na kushinda kombe la Champions League mara mbili, sasa ameshinda makombe yote manne ya mashindano makubwa barani Ulaya.
Ajax Amsterdam, ilikuwa ikicheza kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Ulaya tangu 1996 na kuwasilisha kikosi chenye umri wa miaka 22 na siku 282 kwa wastani, kikosi kinachoelezwa kuwa na wachezaji wenye umri mdogo kabisa kuwahi kucheza katika fainali yoyote ya Ulaya.
Timu hiyo ya kocha Peter Bosz iliitia kishindo Manchester United, lakini haikufaulu kuutikisa wavu. "Bila shaka pande zote ziliathiriwa na shambulizi la Manchester, lakini unapocheza katika fainali, unasahau wakati huo," amesema Bosz. "Nimevunjwa moyo kwa sababu unacheza fainali kushinda. Hatukushinda. Sikuona Ajax niliyoizoweya, kwa maana kwamba kandanda safi, kasi, kushinikiza na kudhibiti mpira. Ilikuwa vigumu kushambulia kwa sababu Manchester United walicheza mipira mirefu na hawakutaka kubahatisha kwa kupanga mchezo. Nadhani haikuwa mechi ya kusisimua." aliongeza kusema.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/reuters/dpae
Mhariri: Mohammed Abdulrahman